Iran imejiunga na kundi la nchi zinazozalisha chanjo ya COVID-19
Msemaji wa Shirika la Dawa na Chakula Iran Daktari Kianoush Jahanpour amesema Iran imejiunga na kundi la nchi chache duniani zinazozalisha chanjo ya corona au COVID-19.
Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter Jumatatu, Daktari Jahanpour aliashiria hatua ya Wizara ya Afya ya Jamhuri ya .Kiislamu ya Iran kuidhinisha matumizi ya dharura ya chanjo ya COVID-19 iliyoundwa hapa nchini ya COV-Iran Barekat na kuandika: "Nchi zinazozalisha chanjo ya COVID-19 duniani sasa ni Iran, Uingereza, India, Russia, China na Marekani."
Waziri wa Afya wa Iran Daktari Saeed Namaki alitangaza Jumatatu kuwa: "Leo idhini ya matumizi ya dharura ya COV-Iran Barekat imetolewa na wiki ijayo pia chanjo ya COVID-19 iliyoundwa na taasisi ya Pasteur ya Iran nayo itapata idhini."
Amesema kwa mujibu wa mipango iliyopo watu wote wanaolengwa nchini Iran wataweza kupata chanjo ya COVID-19 katika kipindi cha miezi sita ijayo.
Hivi karibuni Dkt. Hassan Jalili mkuu wa timu ya utengenezaji chanjo hiyo ya COV-Iran Barekat katika Idara ya Utafiti ya Taasisi ya Utekelezaji wa Maagizo ya Imam Khomeini (MA) alisema kuwa tayari wameshazalisha dozi milioni moja za chanjo hiyo ambayo awamu yake ya tatu ya majaribio imekamilika. Alisema dozi hizo zitakabidhiwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kusambazwa nchini. Amesema hivi karibuni hivi wanatarajia kuzalisha dozi milioni 18 za chanjo ya COV-Iran Barekat.
Iran iko mstari ya mbele kuunda chanjo za COVID-19 ambapo mbali na chanjo ya COV Iran Barakat , chanjo zingine ambazo zimepiga hatua nzuri katika majaribio ni pamoja na Razi Cov Pars, Fakhra na chanjo ya pamoja ya Taasisi ya Chanjo ya Finlay ya Cuba na Taasisi ya Chanjo ya Pasteur ya Iran.