Iran yataka kuondolewa vikwazo taifa la Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i71614-iran_yataka_kuondolewa_vikwazo_taifa_la_syria
Balozi na Naibu Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameitaka jamii ya kimataifa iandae mazingira ya kuondolewa vikwazo vya kikatili dhidi ya taifa la Syria, ambavyo vimewaathiri mno wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 24, 2021 03:22 UTC
  • Iran yataka kuondolewa vikwazo taifa la Syria

Balozi na Naibu Mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameitaka jamii ya kimataifa iandae mazingira ya kuondolewa vikwazo vya kikatili dhidi ya taifa la Syria, ambavyo vimewaathiri mno wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Zahra Ershadi alisema hayo jana Jumatano katika hotuba yake kwa mkutao wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliojadili hali ya kibinadamu nchini Syria.

Ameeleza bayana kuwa, "Sisi kama nchi ambayo imekuwa chini ya vikwazo vya kinyama kwa miongo kadhaa sasa, tunalaani vikwazo vya dawa na chakula, kwa kuwa vitendo vya aina hii havifai, si vya kimaadili na vinakiuka sheria."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza kuwa, kutumiwa mbinu hizo za vikwazo hakujakuwa na matokeo mengine isipokuwa kurefusha muda wa kuhangaika wananchi wa Syria, kuakhirisha kurejea kwa wakimbizi na kuzuia jitihada za kuikarabati na kuijenga upya nchi hiyo iliyokumbwa na vita na mapigano.

Naibu Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, suala la kuondolewa vikwazo vya upande mmoja linapaswa kupewa kipaumbele katika mazungumzo juu ya hali ya kibinadamu kwenye mgogoro wa Syria.

Hali mbaya ya kibinadamu inayoakabiliwa wananchi wa Syria hususan wanawake na watoto wadogo

Mapema jana pia katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Zahra Ershadi alivitaja vikwazo vya upande mmoja vya Marekani kama kizingiti cha kupatikana amani na ustawi duniani.

Amesema Marekani inapasa kukomesha muenendo wake wa kutumia vikwazo na mashinikizo ya upande mmoja kuyaburuza mataifa mengine, na kwamba inafaa kuheshimu wajibu wake wa kimataifa kwa kuheshimu sheria za kimataifa na Hati ya Umoja wa Mataifa.