Rouhani: Kila mwaka Iran huchimbua tani milioni 590 za madini nchini
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kila mwaka Iran huchimbua tani 590 za madini nchini na hivyo sekta hii ina nafasi muhimu katika kubuni ajira kwa vijana.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo mjini Tehran wakati akifungua miradi kadhaa ya Wizara ya Madini na Biashara kwa njia ya video. Rouhani amesema miradi ambayo ameifungua leo inahusiana na sekta ya viwanda na madini.
Rais wa Iran ameongeza kuwa, katika sekta ya madini na viwanda vya madini, kumefanyika kazi kubwa ambayo imeibua nafasi nyingi za ajira na pato sambamba na kukidhi mahitaji ya ndani na nje ya nchi.
Rais Rouhani aidha amesema kuwa katika sekta ya chuma, leo Iran imeweza kujitosheleza na hivyo mbali na kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi inauza bidaa hiyo katika soko la kimataifa.
Rais wa Iran amesema katika miaka minane ya serikali yake inayoondoka, kumefanyika kazi kubwa katika ustawi wa sekta ya madini na viwanda vya madini.
Uzinduzi huo wa miradi ya sekta ya madini leo ni wa 77 tokea rais Rouhani aanzishe uzinduzi wa miradi ya maendeleo kila Alhamisi kote nchini kwa njia ya video.