Khateebzadeh: Misimamo ya Iran kuhusu JCPOA haibadiliki kwa kubadilika serikali
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i72046-khateebzadeh_misimamo_ya_iran_kuhusu_jcpoa_haibadiliki_kwa_kubadilika_serikali
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kuwa, kubadilika kwa serikali hakutasababisha mabadiliko yoyote katika misimamo ya Iran kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jul 06, 2021 03:41 UTC
  • Saeed Khatibzadeh
    Saeed Khatibzadeh

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kuwa, kubadilika kwa serikali hakutasababisha mabadiliko yoyote katika misimamo ya Iran kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Saeed Khatibzadeh ambaye alikuwa akijibu matamshi ya baadhi ya maafisa wa nchi za Ulaya wanaodai kuwa, ili kufikia mapatano kuhusu JCPOA, kuna ulazima wa kusubiri hadi rais mteule wa Iran atakaposhika madaraka, amesema kuwa, msimamo wa Iran kuhusu makubaliano hayo haubadiliki kwa kubadilika uongozi wa nchi.

Kuhusu mazungumzo ya Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA huko Vienna, Khatibzadeh amesema kuwa, kukamilishwa kwa mapatano ya kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kunategemea idara na azma ya kisiasa ya pande nyingine husika katika makubaliano hayo na kuwa tayari kwao kuchukua maamuzi magumu. Amesema Jamhuri ya Kiislamu inafanya juhudi kubwa kuhakikisha kwamba mazungumzo hayo yanazaa matunda haraka iwezekanavyo na vikwazo vyote vya kidhalimu dhidi ya taifa la Iran vinaondolewa.

Kuhusu shambulizi lililofanywa karibuni na Marekani huko Iraq na Syria, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, Washington inapaswa kutambua kuwa, haitafikia malengo yake kwa kutumia sera za mabavu, na kinyume chake, hali ya Marekani itakuwa mbaya zaidi siku baada ya nyingine katika eneo hili la Magharibi mwa Asia.