Iran: Mazungumzo yetu na Saudi Arabia yanaendelea vizuri
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i72064-iran_mazungumzo_yetu_na_saudi_arabia_yanaendelea_vizuri
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mazungumzo baina ya Iran na Saudi Arabia yanaendelea vizuri na hadi hivi sasa mazungumzo hayo yamefanyika kaika anga ya urafiki na maelewano na tunataraji kuwa mazungumzo hayo yatapunguza kwa kiwango kikubwa hitilafu baina ya pande mbili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 06, 2021 06:51 UTC
  • Iran: Mazungumzo yetu na Saudi Arabia yanaendelea vizuri

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mazungumzo baina ya Iran na Saudi Arabia yanaendelea vizuri na hadi hivi sasa mazungumzo hayo yamefanyika kaika anga ya urafiki na maelewano na tunataraji kuwa mazungumzo hayo yatapunguza kwa kiwango kikubwa hitilafu baina ya pande mbili.

Ali Rabei amesema hayo leo Jumanne mbele ya waandishi wa habari na huku akijibu swali juu ya je mazungumzo kati ya Iran na Saudia yamekwama au yanaendelea; amesema, kipaumbele kikuu cha Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran ni kuwa na uhusiano mzuri na majirani zake, hivyo mazungumzo baina yetu na serikali ya Saudi Arabia yanaendelea kwani suala la usalama na amani katika eneo letu ni muhimu sana kwa Jamhuri ya Kiislamu.

Vile vile amesema: Sisi tunaamini pia kuwa, mazungumzo hasa kati ya mataifa ya umma wa Kiislamu, ndiyo njia pekee bora ya kutatua hitilafu zilizopo na zinazojitokeza baina ya mataifa hayo.

Ali Rabei

 

 

Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaelewa vyema kwamba, kuna baadhi ya mambo hitilafu ni kubwa na ni vigumu kuyapatia ufumbuzi, lakini hakuna kisichoweza kutatuliwa na masuala hayo yanahitaji muda wake maalumu wa kuweza kutatuliwa.

Msemaji wa Serikali ya Iran pia amesema: Tehran itaendelea na mazungumzo hayo hadi itakapopunguza kwa kiwango kikubwa sana hitilafu zilizopo na inaamni kwamba matatizo yaliyopo yatatuka kwani daima tunaamini kuwa, pande mbili zinapokuwa na nia njema ni rahisi kudhamini manufaa ya pamoja na kuondoa matatizo yote yaliyopo. Siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote zimesimama juu ya msingi wa kuimarisha mshikamano na kushirikiana zaidi na zaidi kati ya nchi za eneo husika.