Takht-Ravanchi: Vikwazo vya dawa na vifaatiba ni jinai ya kivita
-
Majid Takht-Ravanchi
Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa vikwazo vya Marekani vinazuia kufikishwa vifaatiba, dawa, teknolojia na ushirikiano wa Iran na taasisi za kifedha za kimataifa na ametoa wito wa kukomeshwa haraka vikwazo hivyo.
Majid Takht-Ravanchi ambaye jana Alkhamisi alikuwa akihutubia kikao cha ngazi ya juu cha Umoja wa Mataifa kuhusu virusi vya HIV na ugonjwa wa Ukimwi, ameashiria maendeleo ya Iran katika sekta ya tiba na afya ya waathirika wa Ukimwi ikiwa ni pamoja na kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kupunguza athari mbaya zinazosababishwa na virusi hivyo na kusema: Licha ya maendeleo hayo lakini Jamhuri ya Kiislamu ingali inasumbuliwa na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani ambavyo vinapingana na malengo ya Umoja wa Mataifa na sheria zinazotawala mahusiano ya kimataifa.
Takht-Ravanchi amesema kuwa, katika kipindi hiki cha maambukizi ya corona vikwazo hivyo vya Marekani vimekuwa na taathira mbaya zaidi kwa sekta ya afya hususan kwa wanawake, watoto watu wazima, watu wenye ulemavu na maradhi maalumu na kutahadharisha kuwa, kuhatarisha afya ya umma ya raia kwa malengo ya kisiasa ni ukiukaji wa sheria na jinai ya kivita na vilevile jinai dhidi ya binadamu inayopaswa kufutiliwa kimataifa.
Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, majukumu ya kimaadili yanailazimisha jamii ya kimataifa kupinga vikali jinai hiyo na kukomesha kabisa vikwazo vya kidhamu vya Marekani dhidi ya taifa la Iran.