Waziri Mkuu wa Syria aonana na Ujumbe maalumu wa Iran mjini Damascus
Waziri Mkuu wa Syria, leo Ijumaa ameonana na ujumbe maalumu wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na kuhimiza kuimarishwa zaidi na zaidi uhusiano wa kibunge baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi ndugu ya Syria.
Ujumbe huo wa Bunge la Iran unaoongozwa na Abbas Golroo ambaye ni Mjumbe wa Usalama wa Taifa na Siasa za Nje za Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran. Katika mazungumzo hayo pande mbili zimetilia mkazo pia wajibu wa kutembeleana viongozi wa nchi hizo mbili za Kislamu kwa manufaa ya mataifa haya mawili ya kambi ya muqawama.
Shirika la habari la IRNA limeripoti leo kuwa, Waziri Mkuu wa Syria, Hussein Arnous, amesema katika mazungumzo hayo kwamba Damascus ina azma yakweli ya kuimarisha ushirikiano wake wa kiuchumi na Tehran pamoja na ustawi katika sekta nyingine kwani uhusiano wa Syria na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni wa kiistratijia na ni muhimu sana.
Vile vile amesema, Tehran na Damascus zimeongeza juhudi za kuwekeana mikataba mipya, kurahisisha utekelezaji wa maafikiano yanayofikiwa na kuondoa vizuri vyote katika utekelezaji wa vipengee vya mikataba inayotiwa saini baina ya nchi hizi mbili.
Kwa upande wake Abbas Golroo ambaye pia ni Naibu wa Mkuu wa Kundi la Urafiki la Bunge la Iran na Syria amesema kuwa, lengo la safari ya ujumbe anaouongoza huko Syria ni ni kuzidisha ushirikiano wa Tehran na Damascus na kutafuta njia za kuondoa vizuizi vyote vilivyopo katika uimaeishaji wa ushirikiano wa pande hizi mbili.
Jana ujumbe huo wa Bunge la Iran ulionana na Faisal al Miqdad, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria mjini Damascus.