Khatibzadeh: Mipaka ya Iran na Afghanistan ina utulivu na ni salama
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, hakuna machafuko wala ukosefu wa amani katika mipaka ya Iran na Afghanistan.
Shirika la habari la IRIB limemnukuu Saeed Khatibzadeh akisema hayo kujibu swali aliloulizwa kuhusu hali ya mipaka ya Iran na vivuko vya kuingia na kutokea Afghanistan wakati huu mapigano yanapoendelea katika nchi hiyo jirani na kuongeza kuwa, mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko salama na ina utulivu kutokana na juhudi za askari wenye ghera wa kulinda mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu na kwamba hakuna matukio yoyote ya uvunjifu wa amani katika mipaka hiyo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, baadhi ya wafanyakazi wa Afghanistan walikimbilia ndani ya ardhi ya Iran katika vivuko vya Islam Qala na Abu Nasr Farahi baada ya kutokea mapigano ndani ya ardhi ya Afghanistan.
Vile vile amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itachukua hatua zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa, misingi ya mipaka, makubaliano kati yake na Afghanistan na kwa kuzingatia asili ya ujirani mwema.