Chanjo ya PastoCoVac ya Cuba na Iran ni bora zaidi duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i75564-chanjo_ya_pastocovac_ya_cuba_na_iran_ni_bora_zaidi_duniani
Mkuu wa Taasisi ya Pasteur ya Iran amesema chanjo ya COVID-19 ya PastoCoVac imebainika kuwa moja kati ya chanjo zenye uwezo mkubwa zaidi wa kinga duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 09, 2021 08:29 UTC
  • Chanjo ya PastoCoVac ya Cuba na Iran ni bora zaidi duniani

Mkuu wa Taasisi ya Pasteur ya Iran amesema chanjo ya COVID-19 ya PastoCoVac imebainika kuwa moja kati ya chanjo zenye uwezo mkubwa zaidi wa kinga duniani.

Akizungumza leo Jumamosi mjini Tehran katika kikao na waandishi habari kuhusu chanjo hiyo ambayo ni mradi wa pamoja wa Iran na Cuba, Alireza Biglari amesema, kirusi cha COVID-19 aina ya Delta kimehatarisha kinga ya mwili na uwezo wa chanjo zote katika kukabiliana na aina hiyo umepungua hadi asilimia 50 na hata chini zaidi kwa chanjo  ya Pfizer. Hata hivyo amesema chanjo ya PastoCoVac imebainika kuwa salama zaidi na isiyo na madhara na pia ni yenye kinga ya juu zaidi duniani hivi sasa.

Biglari amesema chanjo hii ya PastoCoVac ni mradi wa pamoja wa Taasisi ya Finlay ya Cuba na Taasisi ya Pasteur ya Iran na kuongeza kuwa ubora wake ni asilimia 91-92.

Chanjo hii ina dozi mbili za kudungwa na katika awamu mbili za majirabio ilijumuisha watu 44,000 nchini Cuba huku awamu ya tatu ikijumuisha watu 24,000 waliojitolea kote Iran na walio na umri wa zaidi ya miaka 18.

Biglari amebaini kuwa, chanjo hii inajulikana kama Soberana 2 nchini Cuba na PastoCoVac nchini Iran na ni moja ya chanjo salama zaidi duniani pia kwa watoto walio katika umri wa miaka 3-18.

Aidha amebaini kuwa chanjo ya PastoCoVac ina uwezo mkubwa wa kukabiliana na aina mpya za COVID-19 kama vile aina ya Delta na aina ya Afrika Kusini au aina zingine zozote ibuka. Hali kadhalika amesema hivi sasa kunafanyika jitihada za kuhakikisha chanjo hiyo inapata kibali cha Shirika la Afya Duniani.

Chanjo ya PastoCoVac itazalishwa kwa wingi na hivi sasa Iran ina uwezo wa kuzalisha dozi milioni moja kwa wiki.