Mkurugenzi mpya wa IRIB aanza kazi rasmi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i75568-mkurugenzi_mpya_wa_irib_aanza_kazi_rasmi
Leo kumefanyika sherehe za kumuarufisha mkurugenzi mpya wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran (IRIB).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 09, 2021 09:07 UTC
  • Dkt. Peyman Jebeli mkurugenzi mpya wa IRIB
    Dkt. Peyman Jebeli mkurugenzi mpya wa IRIB

Leo kumefanyika sherehe za kumuarufisha mkurugenzi mpya wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran (IRIB).

Dkt. Peyman Jebeli mkurugenzi mpya wa IRIB ameanza rasmi majukumu yake katika sherehe iliyouhudhuriwa na mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu, Spika wa Bunge, maafisa wa kiserikali na kijeshi pamoja na wakurugenzi na wafanyakazi wa IRIB.

Pia katika sherehe hiyo ameenziwa mkurugenzi anayeondoka wa IRIB Ali Askari ambaye amehudhumu kwa muda wa miaka mitano.

Hujjatul Islam wal Muslimin Mohammad Mohammadi Golpeygani, Mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesoma dikrii ya kuteuliwa Dkt. Jebeli.

Mnamo Septemba 29 Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei alimteua Dkt. Peyman Jebeli kuwa Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiisalmu ya Iran.

Dkt. Jebeli akizungumza wakati wa sherehe za kuanza rasmi majukumu

Akizungumza katika hafla ya leo, mkurugenzi mkuu wa zamani wa IRIB Ali Askari amesema wakati ambao adui alilenga uzalishaji vipindi na wakati wa vita laini IRIB, iliweza kuleta matumaini na utanashati katika jamii.

Kwa  upande wake Dkt. Jebeli mkurugenzi mpya wa IRIB  amesema IRIB inapaswa kupanua wigo wa kimataifa na daima iwe na ujumbe kwa dunia.

Aidha amesisitiza kuwa, katika kipindi cha usimamizi wake atatumia uwezo wa wasomi na vijana. Ameongeza kuwa IRIB kama chombo cha kitaifa inapaswa kuwa mhimili wa utambulisho na uadilifu.  Halikadhalika amesema ni lazima kufanyike mabadiliko katika IRIB na kuongeza kuwa, IRIB inapaswa kuwa dhihirisha la huduma za mfumo mtakatifu wa Jamhuri ya Kiislamu.