Amir-Abdollahian: Iran ipo pamoja na Syria kwa nguvu zake zote
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa hili lipo pamoja na bega kwa bega na Syria na kuitaja nchi hiyo ya Kiarabu kama mshirika wa kistratijia wa Iran.
Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake na Rais Bashar al-Assad wa Syria akiwa mjini Damascus baada ya kuwasili nchini humo hapo jana (Jumamosi) ikiwa ni mwendelezo wa safari yake ya kiduru baada ya kuzitembelea Russia na Lebanon.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa, hivi sasa Syria inapitia kipindi cha ustawi na utulivu na kwamba, Iran iko pamoja na taifa hilo na kwa nguvu zake zote kama ilivyokuwa ikifanya wakati wa vita dhidi ya ugaidi.
Katika mazungumzo yake na Rais wa Syria, Amir-Abdollahian amejadiliana na kubadilishana mawazo na kiongozi huyo kuhusiana na uhusiano wa pande mbili, matukio ya kieneo na kimataifa.
Aidha Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, katika majuma ya hivi karibuni kumefikiwa makubaliano muhimu kuhusiana na kustawisha zaidi uhusiano baina ya Tehran na Damascus katika masuala ya kiuchumi, kibiashara na utalii na kwamba, kunafanyika za kutekelezwa kivitendo makubaliano hayo haraka iwezekanavyo na natija yake kuonakana haraka.
Amir-Abdollahian jana aliwasili Damascus mji mkuu wa Syria akitokea Lebanon na kabla ya hapo Russia pia, ambapo alikutana na kufanya mazungumzo pia na viongiz mbalimbali wan chi mbili hizo.