Iran, Russia zasisitiza mazungumzo ya JCPOA yatafanikiwa Iran ikiondolewa vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i76326-iran_russia_zasisitiza_mazungumzo_ya_jcpoa_yatafanikiwa_iran_ikiondolewa_vikwazo
Iran na Russia zimesisitiza kwamba mazungumzo ya pande zilizosalia katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015 yatafanikiwa tu iwapo yatapelekea kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran sambamba na pande zote kutekeleza mapatano hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 29, 2021 23:57 UTC
  • Iran, Russia zasisitiza mazungumzo ya JCPOA yatafanikiwa Iran ikiondolewa vikwazo

Iran na Russia zimesisitiza kwamba mazungumzo ya pande zilizosalia katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015 yatafanikiwa tu iwapo yatapelekea kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran sambamba na pande zote kutekeleza mapatano hayo.

Siku ya Ijumaa, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Baqeri-Kani alikutana na mwenzake wa Russia Sergei Lavrov mjini Moscow.

Baqeri-Kani aliwasili Moscow Alhamisi kuendeleza mazungumzo aliyoyafanya Brussels kujadili njia za kuondoa vikwazo ambavyo vimewekwa na Marekani kinyume cha sheria dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Siku ya Jumatano, Ofisi ya uwakilishi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Ulaya ilitangaza kuwa, kuondolewa vikwazo vyote haramu na visivyo vya kisheria ilivyoekewa Iran ndio ajenda kuu ya mazungumzo ya Brussels kati ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa na mratibu wa kamisheni ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Ali Baqeri-Kani

Baqeri-Kani amebainisha kuwa Russia, China na Iran zina mtazamo wa pamoja kuhusu masuala  ya kieneo na kimataifa ikiwemo kadhia ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA. 

Baqeri-Kani amesema nchi za Ulaya za kundi la P4+1 zinapaswa kufungamana na ahadi zao na kuchukua hatua za kuhakikisha Iran inaondolewa vikwazo vilivyo kinyume cha sheria.

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alitangaza kujiondoa katika mapatano ya JCPOA mnamo Mei mwaka 2018 na kisha baada ya hapo akatangaza kurejesha vikwazo vilivyo kinyume cha sheria dhidi ya Iran.