Kuimarisha uhusiano wa kiuchumi ni kipaumbele cha sera za kigeni za Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amirabdollahian amesema kipaumbele katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ni kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na nchi za dunia hasa nchi jirani.
Amirabdollahian ameyasema hayo Jumapili katika mkutano na Said Mohammad, mshauri wa Rais wa Iran na mkurugenzi wa masuala ya maeneo huru ya kiviwanda na kiuchumi nchini.
Ameongeza kuwa, nchi nyingi zinataka kuwekeza katika maeneo huru ya kibiashara na kiuchumi na halikadhalika Wairani waishio nje ya nchi nao pia wamebainisha azma yao ya kuwekeza katika setka hiyo. Ka msingi huo Amirabdollahian amesema Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran inasisitiza kuhusu ushirikiano katika kuwavutia wawekezaji wa kigeni katika maeneo huru ya kibiashara.
Kwa upande wake, Said Mohammad ameashiria matukio ya hivi karibuni na mafanikio katika maeneo huru ya kiuchumi na kibiashara Iran na kusema maeneo hayo yana uwezo mkubwa wa kustawi na kuwavutia wawekezaji.
Mkurugenzi wa masuala ya maeneo huru ya kiviwanda na kiuchumi nchini Iran aidha ametoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran isirikiane zaidi katika kuwavutia wawekezaji katika sekta hiyo.
Iran ina maeneo kadhaa huru ya kibiashara na kiviwanda ambayo ni pamoja na Qeshm , Chabahar,Aras , Anzali , Arvand , Kish na Maku. Katika maeneo hayo wawekezaji huendesha shughuli zao bila kutozwa ushuru wa juu.