Jan 01, 2022 13:01 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Jenerali Soleimani ndiye shakhsia mkubwa wa Iran, Umma

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH), ndiye shakhsia mkubwa zaidi si tu ndani ya Iran, bali katika Umma wote wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumamosi wakati alipokutana na familia ya Shahidi Soleimani,  kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa pili tangu alipouawa shahidi shujaa huyo wa kupambana na ugaidi.

Ayatullah Khamenei ameeleza kuwa, hii leo mrengo wa muqawama umeimarika zaidi na kupata matumaini makubwa kuliko ilivyokuwa miaka miwili iliyopita, kutokana na kuuawa shahidi jenerali huyo anayeenziwa na wote.

Kiongozi Muadhamu katika mkutano na familia ya Jen. Soleimani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema sifa alizojipamba nazo Shahidi Soleimani kama ya ukweli na uaminifu, zilimpelekea mwanamuqawama huyo awe kigezo na kielelezo chema kwa vijana wa eneo la Asia Magharibi.

Ayatullah Khamenei amesema, "hii leo, Jenerali kipenzi Soleimani, kutokana na jitihada zake, amekuwa nembo ya matumaini, kujiamini, ushujaa, uvumilivu na ushindi katika eneo."

Wananchi wa Iraq katika maandamano ya kuadhimisha mwaka wa pili wa kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qasem Soleimani

Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, hakuna shaka waliofanya mauaji ya kikatili dhidi ya Jenerali Soleimani, kama vile Donald Trump, aliyekuwa rais wa Marekani, watalipa gharama ya jinai hiyo.  

Shahidi Soleimani ambaye Januari 3 mwaka 2020 alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo, aliuliwa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa jeshi la kujitolea la wananchi wa Iraq la al Hashdu-Sha'abi na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kikatili la jeshi la kigaidi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad.

Tags