Kiongozi Muadhamu ashiriki maombolezo ya kumbukumbu ya kufa shahidi Bibi Fatima (SA)
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehudhuria kikao cha usiku wa kwanza cha maombolezo ya kukumbuka siku aliyokufa shahidi Bibi Fatimatu-Zahra (SA) binti kipenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW na mke wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib (as), Imamu wa kwanza wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.
Ayatullah Ali Khamenei amehudhuria marasimu hayo ya kimaanawi katika Husseinia ya Imam Khomeini (MA), hapa mjini Tehran. Maombolezo hayo hayakuwa na hadhira, na yamehudhuriwa tu na Kiongozi Muadhamu na msomaji wa Qurani Tukufu, kwa ajili ya kuzingatia protokali za kiafya za kuzuia msambao wa ugonjwa wa Covid-19.
Mmoja wa Makhatibu wa Swala ya Ijumaa hapa mjini Tehran, Hujjatul Islam wal Muslimin Kazem Seddiqi amesema katika maombolezo hayo kuwa, waja wa Allah waliobarikiwa sana, ni wenye uchu wa kuuawa shahidi.
Seddiqi ameeleza kuwa: Kuuliwa shahidi ni fursa ya kukutana na Allah, na hii ni azma ya kila mja wa Allah aliyebarikiwa. Moja ya mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu ni kuwafundisha wanafunzi adhimu kama Shahidi Soleimani, katika chuo cha kifikra cha Imam Ali na Bibi Fatima (AS).
Chini ya malezi ya baba yake, Bibi Fatima (AS) alifikia daraja la juu katika maarifa, elimu na uchamungu. Katika maisha yake, Bibi huyo mtukufu alifahamika sana kwa ukarimu, kujitolea, subira, uchamungu na kuwasaidia masikini na watu wasiojiweza.
Mtukufu huyo alijulikana kwa lakabu na majina kadhaa ya sifa teule kama Zahra, Siddiqah, Taahirah, Mubaarakah, Batul, Raadhiyah na Mardhiyyah.