Rais Rouhani ataka waungaji mkono magaidi duniani watajwe
Rais Hassan Rouhani wa Iran ametoa mwito wa kufanyika jitihada za pamoja za kupambana na ugaidi kote duniani huku akisisitiza kuwa wanaotoa uungaji mkono wa siri kwa magaidi wanapaswa kutajwa ili kusitisha misaada yao kwa magaidi hao.
Rais Rouhani ameyasema hayo Jumamosi mjini Tehran alipokutana na kufanya mazungumzo na Linas Linkevicius, Waziri wa Mambo wa Nje wa Lithuania. Rais wa Iran amesema: "katika hatua ya kwanza ya kupambana ugaidi hasa kundi la ISIS au Daesh, nchi zinazounga mkono ugaidi na kundi hilo zinapaswa kutambuliwa ili zisitishe misaada ya fedha na silaha za kisasa kwa kundi hilo."
Rais Rouhani aidha amesisitizia umuhimu wa kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizi mbili katika vita dhidi ya ugaidi, misimamo mikali na magendo ya mihadarati.
Rais wa Iran amebainisha kuwa, nchi zote zinapaswa kuonyesha azma imara na ushirikiano katika vita dhidi ya ugaidi. Aidha amesema nchi za dunia zinapaswa kufahamu kuwa, kuunga mkono magaidi na kuwatumia kwa malengo ya kisiasa si chaguo nzuri na halitakua na tija njema.