Mazungumzo ya Vienna; Iran inafuatilia mapatano ya aina gani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80094-mazungumzo_ya_vienna_iran_inafuatilia_mapatano_ya_aina_gani
Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo ya simu na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Joseph Borell, ambapo ametoa tathmini kuhusu hali ya hivi sasa ya mazungumzo ya Vienna na kusema, "Tehran imedhamiria kufikia makubaliano, lakini maslahi ya kitaifa ya Iran lazima yadhaminiwe."
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 07, 2022 17:34 UTC
  • Mazungumzo ya Vienna; Iran inafuatilia mapatano ya aina gani

Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo ya simu na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Joseph Borell, ambapo ametoa tathmini kuhusu hali ya hivi sasa ya mazungumzo ya Vienna na kusema, "Tehran imedhamiria kufikia makubaliano, lakini maslahi ya kitaifa ya Iran lazima yadhaminiwe."

Ameongeza kuwa Iran ina nia ya dhati ya kufikia makubaliano, lakini pia inasisitiza azma ya kulinda mistari yake miekundu na maslahi ya kitaifa. Aidha amesema, "baadhi ya maendeleo chanya yamepatikana katika mazungumzo hayo, lakini bado hayafikii matarajio ya Iran."

Naye Josep Borrell  ambaye ni mratibu mkuu wa mazungumzo ya Vienna amesema,"Mazungumzo ya Vienna yako katika kipindi muhimu na pande zote zina ajenda ya wazi ya kufikia mapatano."

Uzoefu kuhusu mapatano ya JCPOA na kukiukwa utekelezaji wa makubaliano haya na hatimaye kujiondoa Marekani katika JCPOA na kisha kutokuwa na uwezo Ulaya kudhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran katika makubaliano haya ya nyuklia, kumeifanya Iran ishiriki katika duru mpya ya mazungumzo ya kuondoa vikwazo huko Vienna ikiwa na tahadhari zaidi.

Duru mpya ya mazungumzo ya Vienna ilisitishwa Januari 28, 2022, ili kuwezesha jumbe husika kurejea katika miji mikuu kwa ajili ya mashauriano na kuchukuliwa maamuzi ya kisiasa yenye lengo la kufikia makubaliano.

Mazungumzo ya Vienna

Ifahamike kuwa makubaliano ya kuondoa vikwazo yataidhinishwa na Iran wakati tu yataweza kuthibitishwa kuwa yanatekelezeka sambamba na kudhaminiwa kwa uhakika maslahi ya kiuchumi ya Iran bila ya kutegemea sheria za ndani za nchi nyingine, hasa Marekani.

Mapatano ya JCPOA, yaliyofikiwa mwaka 2015 baina ya Iran na nchi za 5+1 pamoja na Umoja wa Ulaya, hadi sasa hayajaweza kudhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran. Aidha sera za Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya kutokuwa na uwezo wa kuchukua hatua au maamuzi nje ya kivuli cha Marekani kumeongeza hali ya Iran kutokuwa na imani na baadhi ya pande nyingine katika mazungumzo ya Vienna.

Katika mazingira kama hayo, Iran itaafiki tu makubaliano ambayo kwa uhalisia na kiuendelevu yanakidhi maslahi yake kiuchumi, na hivyo haitosheki na yaliyo kwenye karatasi pekee.

Mapatano ya JCPOA yalitiwa saini na kuanza kutekelezwa mwaka 2015 kwa lengo la kudhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran mkabala wa kuwepo baadhi ya vizingiti katika mpango  wake wa nyuklia. Hata hivyo, sio tu kwamba maslahi haya hayakudhaminiwa kwa njia endelevu, bali kwa kujiondoa Marekani kutoka JCPOA, vikwazo vipya dhidi ya Iran viliwekwa.

Kutokuwa na imani na upande wa pili kumeifanya timu ya mazungumzo ya Iran katika duru mpya ya mazungumzo kuwasilisha mapendekezo ya njia za utatuzi wa  kimantiki huku ikitathmini namna upande wa pili unavyolipa suala hili uzito. Aidha Iran inalenga kuhakikisha kuwa iwapo makubaliano yatafikiwa ipate dhamana ya kuzuia kukiukwa tena maslahi yake ya kitaifa.

Maadamu Iran haitapata hakikisho kuhusu msingi huu muhimu, hakuna makubaliano yatakayofikiwa huko Vienna.

Ni katika fremu hiyo hiyo ndio; Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akaandika katika ukurasa wa Twitter siku ya Jumamosi kuwa: "Manufaa ya kiuchumi ya kweli, yenye ufanisi na yanayoweza kuthibitishwa kwa Iran ni sharti la lazima kwa ajili ya kufikiwa mapatano."

Ali Shamkhani

Uuzaji wa mafuta bila usumbufu na Iran kuruhusiwa kupokea nchini mapato yake ya kigeni kwa njia endelevu, ushirikiano usio na kikomo wa benki za Irani na benki za kigeni, mchakato usio na matatizo wa biashara ya nje ya Iran bila kujali ni serikali gani inaingia madarakani nchini Marekani, pamoja na uwekezaji imara wa kigeni na wa kutegemewa ndani ya Iran, ni kati ya  nukta ambazo upande wa pili unapaswa kutoa dhamana ya kuzitimiza  ili ipatikane njia ya kufikia makubaliano katika duru mpya ya mazungumzo ya Vienna.