Iran: Kumalizika mazungumzo ya Vienna kunategemea kuondolewa vikwazo Tehran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema muda wa kumalizika mazungumzo ya Vienna ya kujaribu kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA unategemea irada ya Wamagharibi ambao ni upande wa pili wa mazungumzo hayo, kuiondolewa vikwazo haramu Tehran.
Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Alkhamisi hapa mjini Tehran, katika hafla iliyofanyika kwa mnasaba wa kumbukumbu ya miaka 43 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa, katika kipindi chote cha historia, Wairani wameonesha kuwa huwa wanajibu vitisho kwa muqawama na uvumilivu.
Amesema wakati wa kufikia tamati mazungumzo ya Vienna upo mikononi mwa nchi za Magharibi, kwani ndizo zitakazoamua ni lini zitaliondolea vikwazo taifa la Iran, na zirejee katika kutekeleza wajibu wao kwenye mapatano hayo ya kimataifa.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza kuwa, Iran ina azma na irada ya kweli ya kufikia mapatano mazuri kwenye mazungumzo hayo ya Vienna, na imethibitisha hilo kivitendo.
Wawakilishi wa Iran na kundi la 4+1 linalojumuisha China, Russia, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Umoja wa Ulaya wanaendelea na mazungumzo ya kuondoa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu huko Vienna nchini Austria.
Ijumaa iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alitia saini idhini ya kuondolewa vikwazo kadhaa vya nyuklia vinavyohusiana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA; hatua ambayo Tehran inasisitiza kuwa haitoshi.