Shamkhani: Mienendo hasi ya US ndilo tishio kuu kwa mapatano yoyote yale
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80402-shamkhani_mienendo_hasi_ya_us_ndilo_tishio_kuu_kwa_mapatano_yoyote_yale
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema siri ya kufikiwa mapatano mazuri kwenye mazungumzo ya kuiondolea vikwazo haramu Jamhuri ya Kiislamu ni Tehran kupewa dhamana ya kisheria ambayo itaifanya Marekani isiweze kujitoa kwa mara nyingine tena ndani ya mapatano ya JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 15, 2022 23:17 UTC
  • Shamkhani: Mienendo hasi ya US ndilo tishio kuu kwa mapatano yoyote yale

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema siri ya kufikiwa mapatano mazuri kwenye mazungumzo ya kuiondolea vikwazo haramu Jamhuri ya Kiislamu ni Tehran kupewa dhamana ya kisheria ambayo itaifanya Marekani isiweze kujitoa kwa mara nyingine tena ndani ya mapatano ya JCPOA.

Ali Shamkhani alisema hayo jana Jumanne katika ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa Twitter na kusema kuwa, kuwepo hakikisho la kudumu makubaliano hayo, na uthibitisho wa kuondolewa vikwazo ndio matakwa mawili makuu ya Iran ya kutekeleza tena kikamilifu makubaliano ya JCPOA.

Amesema kuna udharura kwa nchi za Magharibi kutoa hakikisho kuwa zitafungamana kikamilifu na makubaliano hayo, ambayo yalianza kuyumba baada ya Marekani kujiondoa kwayo mnamo Mei mwaka 2018.

Admeri Shamkhani amesema ni jambo lililothibiti kuwa, mienendo hasi ya Marekani ndilo tishio kubwa zaidi kwa mapatano yoyote yale.

Mazungumzo ya Vienna

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameongeza kuwa, "Kuondolewa ya kweli vikwazo kuna maana kwamba, Iran itaweza kufurahia manufaa ya uchumi endelevu na wenye itibari."

Duru ya nane ya mazungumzo ya uondoaji vikwazo ilianza mjini Vienna tarehe 27 Desemba; na baada ya kusitishwa kwa kipindi kifupi ili pande husika ziende kufanya mashauriano katika miji yao mikuu, ilianza tena tarehe 8 ya mwezi huu wa Februari, katika mji mkuu huo wa Austria.