Iran, Russia, China zapinga kutumiwa vibaya kadhia ya haki za binadamu
Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Iran amekutana na mabalozi wa Russia na China nchini Iran ambapo wametangaza kwa pamoja kupinga kutumiwa vibaya kadhia ya haki za binadamu kama chombo cha kuyashinikiza mataifa mengine.
Levan Dzhagaryan, Balozi wa Russia, na Chang Hua, Balozi wa China nchini Iran wamekutana kwa nyakati tafauti na Kazem Gharibabadi Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Iran ambaye pia ni mkuu ya masuala ya kimataifa katika Idara ya Mahakama ya Iran.
Katika mikutano hiyo, Gharibabadi ameashiria ushirikiano wa kistratijia baina ya Iran , Russia na China huku akisisitiza haja ya kustawisha ushirikiano katika nyanja za sheria, uadilifu na haki za binadamu.
Aidha ameunga mkono pendekezo la Russia kuhusu kuendelea kupinga maazimio ya haki za binadamu dhidi ya Iran. Kwa upande wake balozi wa China amesema matukio ya kisiasa na kimataifa hayawezi kubadili irada ya nchi yake katika kushirikiana na Iran. Amesema China inalaani vikali hatua ya madola ya Magharibi kuingilia mambo ya ndani ya Iran kwa visingizio vya haki za binadamu.
Maafisa hao wa Iran, Russia na China wametangaza kwa kauli moja kuwa wanapinga kutumiwa vibaya kadhia ya haki za binadamu kama chombo cha kuzishinikiza nchi zingine na wamesisitiza kuhusu haja ya kuendelea na mashauriano katika ngazi za maafisa wa nchi na pia katika ngazi ya kimataifa.