Shamkhani: Mgogoro wa Ukraine unapaswa kuwa funzo kwa madola ya Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80748-shamkhani_mgogoro_wa_ukraine_unapaswa_kuwa_funzo_kwa_madola_ya_magharibi
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, nchi za Magharibi inabidi zipate funzo katika mgogoro wa Ukraine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 25, 2022 03:26 UTC
  • Shamkhani: Mgogoro wa Ukraine unapaswa kuwa funzo kwa madola ya Magharibi

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, nchi za Magharibi inabidi zipate funzo katika mgogoro wa Ukraine.

Tarehe 21 mwezi huu wa Februari, Rais Vladirimir Putin wa Russia alizilaumu nchi za Magharibi kwa kuchochea machafuko na kutozingatia wasiwasi wa Moscow kuhusu usalama wake wa kitaifa hivyo aliamua kutambua uhuru wa majimbo mawili ya Donetsk na Luhansk yaliyotangaza kujitenga na Ukraine.

Mapema jana asubuhi, Rais Vladimir Putin alitoa hotuba kwenye televisheni na kutangaza kuwa Russia imeamua kufanya operesheni maalumu ya kijeshi katika eneo la Donbas ili kuifanya Ukraine isiwe eneo la kijeshi na wala hakuwa na nia ya kukalia kwa mabavu ardhi ya nchi hiyo.

Vita nchini Ukraine

 

Eneo la Donbas liko mashariki mwa Ukraine na mbali na majimbo ya Donetsk na Luhansk kuna sehemu nyingine kadhaa ambazo wananchi wake ni Warusi, zimo kwenye eneo hilo la Donbas. Mwaka 2014 majimbo ya Donetsk na Luhansk yalitangaza kujitenga na Ukraine kutokana na wafuasi wa nchi za Magharibi wanaoichukia Russia kutwaa madaraka Kyiv, mji mkuu wa Ukraine.

Shirika la habari la Tasnim limemnukuu Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisema kwenye ujumbe wake huo wa Twitter kwamba, kuporomoka masoko ya fedha na kupanda gharama za nishati kutokana na mgogoro wa eneo la mashariki kabisa la bara Ulaya ni uthibitisho kwamba kuchochea machafuko na kukosekana utulivu katika eneo hilo kuna taaathira kubwa hasi kwa nchi za Magharibi.