Mauzo ya mafuta ya Iran nje ya nchi yaongezeka kwa 40%
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema uuzaji wa mafuta yake katika soko la kimataifa umeongezeka kwa asilimia 40 katika kipindi cha miezi mitano iliyopita, licha ya vikwazo dhidi ya taifa hili.
Hayo yamesemwa na Ehsan Khandouzi, Waziri wa Uchumi na Fedha wa Iran katika mahojiano na televisheni ya al-Alam na kuongeza kuwa, vikwazo shadidi vya Marekani na waitifaki wake wa Magharibi vimeshindwa kupunguza mauzo ya mafuta ya Iran nje ya nchi kama walivyokusudia.
Amebainisha kuwa, ingawaje kwa kiasi fulani vikwazo hivyo vya Wamagharibi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita vimeathiri ustawi wa uchumi wa Iran, lakini taifa hili limefanikiwa kugundua fursa mpya katika kitovu cha mashinikizo hayo ya kiuchumi.
Waziri wa Uchumi na Fedha wa Iran amesema vyovyote yakakavyokuwa matokeo ya mazungumzo ya kujaribu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA huko Vienna, lakini Tehran itaendelea kuwa na nafasi ya kipekee katika masoko ya mafuta na gesi duniani.

Wizara ya Mafuta ya Iran imechukua hatua za lazima ikitumia suhula na nyenzo zote katika sekta ya nishati kwa ajili ya kuongeza kasi ya kuzalisha na kuuza mafuta nje ya nchi kulingana na uwezo uliopo.
Wadadisi wa mambo wanasisitiza kuwa, ni jambo lisilowezekana kufikisha mauzo ya mafuta ya Iran kwenye kiwango cha sifuri, licha ya vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi.