Khatibzadeh: Hatuko Vienna kwa ajili ya kufikia makubaliano mapya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80866-khatibzadeh_hatuko_vienna_kwa_ajili_ya_kufikia_makubaliano_mapya
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Saeed Khatibzadeh amesema kuwa, ushiriki wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya Vienna si kwa ajili ya kufikia makubaliano mapya na kueleza kuwa, hali ya hivi sasa si ya utata kwa Washington na Ulaya, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitavuka mistari yake myekundu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 28, 2022 10:05 UTC
  • Saeed Khatibzadeh
    Saeed Khatibzadeh

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Saeed Khatibzadeh amesema kuwa, ushiriki wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya Vienna si kwa ajili ya kufikia makubaliano mapya na kueleza kuwa, hali ya hivi sasa si ya utata kwa Washington na Ulaya, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu haitavuka mistari yake myekundu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tehran mapema leo Jumatatu, Khatibzadeh ameashiria msimamo wa Iran kuhusu masuala yaliyosalia katika mazungumzo ya Vienna na kusema: Kiongozi wa timu ya mazungumzo ya Iran, Ali Bagheri Kani alirejea Tehran kufanya mashauriano yanayohitajika katika masuala yaliyosalia, na Baraza la Usalama wa Kistratejia la Taifa linasimamia masuala yaliyosalia likiongozwa na Rais wa Jamhuri. 

Ameongeza kuwa: "Tumezieleza nchi za Magharibi kuhusu mistari yetu myekundu na tunaamini kwamba, Washington na Ulaya wameelewa vyema mistari hiyo, na tunatarajia pande nyingine hazitarefusha tena mazungumzo."

Kuhusu taathira za vita vya Ukraine kwenye mazungumzo ya Vienna, Khatibzadeh amesema: Hakuna uhusiano kati ya mazungumzo hayo na vita vya Ukraine na Russia; yanayojiri Vienna yanahusiana na makubaliano ya nyuklia na maslahi ya pande zote zinazohusika.

Msemaji wa Wizara yya Mambo ya Nje ya Iran ametilia mkazo umuhimu wa kuendelezwa mazungumzo baina ya Russia na Ukraine kwa ajili ya kukomesha vita na kutafuta suluhisho la kisiasa la mgogoro huo.