Iran yalaani shambulio la roketi la Israel dhidi ya Damascus, Syria
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali shambulizi la roketi la utawala haramu wa Israel dhidi ya mji mkuu wa Syria, Damascus.
Saeed Khatibzadeh amesema Jamhuri ya Kiislamu imesikitishwa mno na hujuma hiyo iliyoua askari wawili wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ambao walikuwa walinzi wa Haram Tukufu.
Khatibzadeh ameeleza bayana kuwa, kitendo hicho cha kipumbavu cha utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unapenda kufanya mauaji hata dhidi ya watoto, hakitapita hivi hivi bila kupewa jibu mwafaka.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, "mzizi wa jinai ya namna hii umetokana na dhati na hulka ya utawala wa Kizayuni wa kupenda kuvamia, kukalia kwa mabavu na kufanya ugaidi."
Vikosi vya ulinzi wa anga vya Syria jana vilifanikiwa kuzuia na kutungua maroketi yaliyorushwa na jeshi la Israel katika maeneo mbalimbali karibu na Damascus, lakini moja liliua askari wawili wa SEPAH, waliokuwa walinzi wa Haram Tukufu.
Serikali ya Syria imeonya kuwa vitendo hivyo vya kichokozi vya utawala pandikizi wa Israel vinaweza kuvuruga utulivu wa eneo na amani na usalama wa kimataifa.
Utawala wa Kizayuni daima hulenga maeneo ya jeshi na miundombinu ya Syria katika kuwaunga mkono magaidi wanaoendesha mashambulizi kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Bashar al-Asad wa nchi hiyo.