Amir-Abdollahian: Kustawisha uhusiano na Russia kuna umuhimu kwa Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, bila kujali matukio na mabadiliko yoyote yanayojiri kimataifa, kustawisha uhusiano na Russia kuna umuhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, leo mchana alielekea wizara ya mambo ya nje ya Russia kwa mazungumzo na waziri mwenzake Sergey Lavrov baada ya kuwasili mjini Moscow akiongoza ujumbe maalumu wa ngazi ya juu wa wizara yake.
Katika mazungumzo hayo, Amir-Abdollahian ameeleza furaha yake ya kuwepo mjini Moscow na akasema: tunashukuru kutokana na jitihada chanya na athirifu zinazofanywa na wajumbe wa Russia katika mazungumzo ya Vienna ili kusaidia kufikia makubaliano kwa ajili ya kuondolewa vikwazo ilivyowekewa Iran.
Halikadhalika, waziri wa mambo ya nje wa Iran amesema, leo imepatikana fursa muhimu ya kuzungumza na kushauriana kuhusu matukio ya Ukraine, Afghanistan, Yemen, Syria, Palestina na masuala mengine ya kimataifa.
Katika mazungumzo hayo na waziri wa mambo ya nje wa Iran, Sergey Lavrov amesema, mazunguzo ya Vienna yanakaribia kukamilika na akaongeza kuwa uhusiano wa kibiashara wa Iran na Russia umevunja rekodi ambapo mwaka uliopita uliongezeka kwa asilimia 80.
Mara baada ya kuwasili mjini Moscow, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema: "sisi tunalaani kwa uwazi kabisa vita, viwe vya Ukraine, Afghanistan, Yemen na mahali pengine popote pale duniani' na akaongeza kuwa, Iran inajikita katika kutafuta njia ya ufumbuzi wa kisiasa katika kadhia ya Ukraine.../