Iran: Tutaishambulia tena Israel kwa makombora ikituchokoza
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ametahadharisha kuwa, iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utafanya tena vitendo vyake vya kishetani dhidi ya Iran, basi uwe tayari kukabiliwa tena kwa makombora ya balestiki ya jeshi la SEPAH.
Meja Jenerali Hossein Salami alitoa indhari hiyo jana Jumatano akihutubia hafla ya kitamaduni katika mji wa Dezful kusini magharibi mwa Iran na kusisitiza kuwa, utawala huo haramu unapaswa kuachana na mienendo yake ya kitwaghuti mmbele ya Iran.
Kamanda Salami amebainisha kuwa, iwapo utawala pandikizi wa Israel utakosea tena katika mahesabu yake, basi utaandamwa tena na vipigo vya nguvu na vya kuumiza.
Amesema: Jeshi la SEPAH haliwaziki tu mashahidi wake, lakini pia hujibu chokochoko na kulipiza kisasi cha damu za mashahidi hao.
Hivi karibuni, kambi mbili za kutoa mafunzo za Shirika la Ujasusi la Israel (MOSSAD) zilishambuliwa kwa makombora ya balestiki na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran katika mji wa Erbil, eneo la Kurdistan kaskazini mwa Iraq.
SEPAH ilisema imefanya operesheni hiyo kufuatia jinai za hivi karibuni za utawala bandia wa Israel, na tangazo la hapo awali na IRGC la kutonyamazia kimya jinai za utawala huo.