Mkuu wa IRGC: Maadui wanaogopa jibu zito la Iran
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) amesema kosa lolote dogo katika kuamiliana na Iran litaibua jibu zito, na kwa msingi huo maadui hawana uthubutu na ujasiri wa kuitunishia misuli Jamhuri ya Kiislamu.
Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa IRGC ameyasema hayo leo Jumatatu akizungumza na waandishi wa habari katika mji wa Khoramshahr, Kusini Magharibi mwa Iran na kuongeza kuwa, maadui wanapaswa kufutilia mbali fikra zao ghalati, kwani jibu la taifa hili kwa chokochoko za maadui litakuwa zito.
Amesisitiza kuwa, maadui wanapaswa kutambua kwamba, majibu ya Iran kwa uchokozi wowote wa maadui yatakuwa haribifu, ya kusambaratisha na ya kuwafanya wajute.
Meja Jenerali Salami sambamba na kuwaenzi mashahidi wa taifa hili waliojitoa muhanga kwa ajili ya uhuru wa nchi hii amesema, "Hii leo, nguzo za uwezo wa Iran ni madhubuti, na Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kung'ara duniani."
Kamanda Mkuu wa Jeshi la SEPAH la Iran ameongeza kuwa, maadui hawatakuwa na chaguo jingine isipokuwa ama kuwa tayari kulipa gharama iwapo wataamua kubakia (katika eneo hili) au wasubiri kupata fedheha kwa kulazimika kukimbia.