Mkuu wa IRGC atahadharisha kuhusu shughuli za Israel katika Ghuba ya Uajemi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i81984-mkuu_wa_irgc_atahadharisha_kuhusu_shughuli_za_israel_katika_ghuba_ya_uajemi
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amezionya baadhi ya nchi za Kiarabu kwamba uwepo wa Israel katika eneo la kistratijia la Ghuba ya Uajemi ni sababu ya ukosefu wa usalama, na amezitaka zisitishe ushirikiano wao na utawala huo ghasibu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 31, 2022 03:30 UTC
  • Meja Jenerali Hossein Salami
    Meja Jenerali Hossein Salami

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amezionya baadhi ya nchi za Kiarabu kwamba uwepo wa Israel katika eneo la kistratijia la Ghuba ya Uajemi ni sababu ya ukosefu wa usalama, na amezitaka zisitishe ushirikiano wao na utawala huo ghasibu.

Meja Jenerali Hossein Salami aliyekuwa akizungumzia hali ya usalama katika Ghuba ya Uajemi, Mlango-Bahari wa Hormuz na Bahari ya Oman, ametahadhari kuhusu harakati za Israel katika eneo hilo la kistratijia.

Amesema inasikitisha kwamba baadhi ya tawala za Kusini mwa Ghuba ya Uajemi zimeanzisha uhusiano wa kisiasa na kiusalama na utawala wa Kizayuni, jambo ambalo ni tishio kubwa kwa usalama wa eneo hili na kwa tawala hizo zenyewe.

Ameonya kwamba kuendelea kwa mahusiano kama haya hakukubaliki hata kidogo.

Kamanda Mkuu wa IRGC ameyaonya mataifa ya kikanda kwamba uwepo wa Israeli ni chanzo cha ukosefu wa usalama sio tu katika Ghuba ya Uajemi bali pia katika eneo lolote unapotia mguu.

Onyo la Meja Jenerali Salami limetolewa baada ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Morocco - nchi tatu za Kiarabu ambazo mwaka 2020 zilianzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Israel kwa ushawishi wa Marekani- kukutana katikka eneo linalokaliwa kwa mabavu la Naqab (Negev) ili kuendeleza uhalalishaji wa uhusiano wao na utawala huo haramu.

Wakati huo huo Meja Jenerali Hossein Salami ameashiria hali nzuri na nguvu za kivita za vitengo na vikosi vya IRGC, hususan vile vilivyotumwa katika visiwa muhimu vya Kusini mwa Iran, na vilevile utayarifu wao wa kutetea maeneo ya Jamhuri ya Kiislamu mbele ya vitisho vinavyoweza kutokea.