Khatibzadeh: Marekani bado haijaonyesha nia ya kufikia makubaliano
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82386-khatibzadeh_marekani_bado_haijaonyesha_nia_ya_kufikia_makubaliano
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema kuwa, Marekani bado haijaonyesha nia ya kutosha ya kufikia makubaliano katika mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea huko Vienna nchini Austria na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiathiriwi na kampeni za vyombo vya habari na matamshi yanayokinzana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 11, 2022 03:48 UTC
  • Saeed Khatibzadeh
    Saeed Khatibzadeh

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema kuwa, Marekani bado haijaonyesha nia ya kutosha ya kufikia makubaliano katika mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea huko Vienna nchini Austria na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiathiriwi na kampeni za vyombo vya habari na matamshi yanayokinzana.

Saeed Khatibzadeh ameyasema hayo mapema leo katika kikao chake cha kila wiki na waandishi wa habari na kuongeza kuwa: Maslahi ya wananchi wa Iran ndio mwanga na dira ya kazi za viongozi wote.

Amesema matini ya makubaliano haijakamilishwa na kwamba mazungumzo yanaendelea kwa mkakati wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa na utekelezaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni.

Khatibzadeh amesema kwamba ikiwa mistari myekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ingezingatiwa katika mazungumzo ya Vienna kungefikiwa makubaliano miezi kadhaa iliyopita, na kuongezsa kuwa pande zinazohusika katika mazungumzo hayo bado hazijafikia mahali ambapo upande wa Marekani utaonyesha kuwa unatekeleza majukumu na wajibu wake.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema: "Marekani inajaribu kutumia nguvu na wakati wa pande zote kwa ajili ya kudumisha vipengele vya mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Iran, lakini lililo muhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ni manufaa ya kiuchumi na maslahi ya wananchi wa Iran kupitia njia ya kuondolewa vikwazo."

Khatibzadeh

Kuhusu suala la kusimamishwa uanachama wa Russia katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Haki za binadamu ni jambo lenye thamani kubwa ambalo halipaswi kutolewa muhanga kwa ajili ya  masuala ya kisiasa.

Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipinga muswada wa nchi za Magharibi wa kutaka kusimishwa uanachama wa Russia katika Baraza la Haki za Binadamu la UN kwa sababu inaamini kwamba haki za binadamu hazipaswi kufanywa muhanga wa masuala ya kisiasa.