Iran: Tumejiandaa kikamilifu kukabiliana vilivyo na vitisho vya maadui
Kamanda wa Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema kuwa, majeshi ya Jamuri ya Kiislamu ya Iran yako imara na yamejiandaa kikamilifu kukabiliana vilivyo na vitisho vya maadui.
Shirika la habari la Mehr limemnukuu Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour akisema hayo leo wakati akifanya ziara katika makaburi ya mashahidi mjini Kerman, kusini mwa Iran na kuwaambia waandishi wa habari kwamba, wanamapambano waliopigana bega kwa bega na Luteni Jenerali shahid Qassem Soleimani, Kamanda wa Zamani wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH bado wako imara katika kulinda mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Brigedia Jenerali Pakpour pia amekumbushia ulipizaji kisasi mkali uliotolewa na jeshi la SEPAH baada ya wanajeshi magaidi wa Marekani kumuua kidhulma na kiwogawoga Luteni Jenerali Soleimani na kusema, maadui hawana tena uwezo wa kuishambulia na kuivamia Jamhuri ya Kiislamu.
Itakumbukwa kuwa tarehe 3 Januari 2020, wanajeshi magaidi wa Marekani waliushambulia msafara wa Luteni Jenerali Qassem Soleimani akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Iraq na kumuua shahidi kidhulma tena uraiani. Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliuawa kigaidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq maarufu kwa jina la al Hashd al Shaabi pamoja na watu wengine wanane waliokuwemo kwenye msafara huo karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad, Iraq.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH lilitoa majibu makali kwa wanajeshi magaidi wa Marekani kwa kuipiga kwa makombora na kuisambaratisha kambi yao ya kijeshi ya Ain al Assad huko Iraq.