Jun 01, 2022 09:58 UTC
  • Iran yajibu matamshi ya Ufaransa, Ujerumani kuhusu meli za mafuta za Ugiriki

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa taarifa na kukosoa taarifa zinazofanana za Ujerumani na Ufaransa kuhusu meli za mafuta za Ugiriki.

Siku ya Ijumaa Idara Kuu ya Mahusiano ya Umma ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ilitangaza kuwa meli mbili za mafuta za Ugiriki zilikamatwa katika maji ya Ghuba ya Uajemi kwa sababu ya kukiuka taratibu. 

Kuhusiana na nukta hii Msemaji wa Wzara ya Nje ya Ufaransa ametoa taarifa na kuitaka Iran iachilie huru meli hizo mara moja na kutekeleza majukumu yake ya sheria za kimataifa kuhusu uhuru wa ubaharia. Katika upande mwingine Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani naye pia ametoa taarifa sawa na hiyo na kuitaka Iran iachilie huru meli hizo za Ugiriki.

Kuhusiana na taarifa hizo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Saeed Khatibzadeh amesema Iran haizikubali hata kidogo taarifa kama hizo za upande mmoja ambazo sasa imekuwa ni ada kutolewa na nchi hizo.

Khatibzadeh amesema badala ya nchi hizo kuunga mkono ukiukwaji uliotekelezwa na meli hizo za Uguriki, zinapaswa kuunga mkono mkondo wa sheria ambao unaenda sambamba na sheria za kimataifa kwa lengo la kudhamini usalama na uhuru wa meli za kibiashara kuendesha shughuli zao baharini.

Khatibzadeh amesema inasikitisha kuona kuwa nchi hizo zinadai hatua ambayo Iran imechukua ni kinyume cha sheria lakini zimenyamazia kimya kitendo kilicho kinyume cha sheria cha Ugiriki ambapo nchi hiyo iliisimamisha meli ya mafuta iliyokuwa na bendera ya Iran na kisha kuyahamisha mafuta yaliyokuwa kwenye meli hiyo na kuyapa meli ya nchi nyingine.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema badala ya wakuu wa Uigiriki kuanzisha chokochoko za kisiasa na kipropaganda kutatua kadhia hiyo wanapaswa kufuatilia suala la meli hizo kupitia njia za kisheria na za mahakama nchini Iran.

Tags