Iran: Tutachukua hatua zinazofaa kukabiliana na hatua za kiadui za IAEA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84458-iran_tutachukua_hatua_zinazofaa_kukabiliana_na_hatua_za_kiadui_za_iaea
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, muswada wa azimio la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kwa Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa haikubaliki kabisa na kwamba Tehran itajibu inavyofaa hatua hiyo ya IAEA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 06, 2022 22:02 UTC
  • Iran: Tutachukua hatua zinazofaa kukabiliana na hatua za kiadui za IAEA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, muswada wa azimio la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kwa Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa haikubaliki kabisa na kwamba Tehran itajibu inavyofaa hatua hiyo ya IAEA.

Kikao cha Bodi ya Magavana ya wakala wa nyuklia wa IAEA kilianza jana Jumatatu katika makao ya wakala huo huko Vienna Austria.

Marekani na nchi tatu za Ulaya za Ujerumani, Uingereza na Ufaransa zimetoa pendekezo la pamoja kwa bodi hiyo na kuda kuwa eti zina wasiwasi mkubwa na mada za urani ambazo eti zimepatikana katika maeneo ya nyuklia ambayo zimedai hayakutangazwa na Iran.

Nchi hizo nne za Magharibi zimedai pia kuwa, eti Iran imeshindwa kutoa ushirikiano wa kutosha, kuna mambo bado hayajapatiwa ufumbuzi na kuitaka Iran ifanye haraka kuongeza ushirikiano wake na IAEA kuweza kutatua masuala yaliyobakia.

Bodi ya Magavana ya IAEA

 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh amekanusha madai yote hayo ya nchi nne za Magharibi na kusema katika mahojiano kwa njia ya televisheni kwamba hivi sasa Tehran haisemi chochote maadamu Bodi ya Magavana ya IAEA haijawasilisha bado muswada wake wa kiuadui dhidi ya Iran mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Lakini iwapo bodi hiyo itawasilisha muswada huo, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo itachukua hatua zinazofaa kujibu uadui wa madola hayo manne ya Magharibi dhidi yake.

Amesema, tangu zamani Iran inashirikiana vizuri tu na Wakala wa Kimataifa wa Nyuklia wa IAEA kiasi kwamba tangu tarehe 5 Machi 2022 hadi hivi sasa, kumeshafanyika vikao vitatu kati ya Iran na IAEA lakini inashangaza kuona Mkurugenzi Mkuu wa IAEA anategemea madai ya uongozo ya utawala pandikizi wa Israel katika ripoti yake.

Amewataka wanachama wote wa IAEA kuchukua tahadhari katika misimamo na maamuzi yao na wasiingize siasa katika masuala ya kiufundi.