Shamkhani: Iran inataka makubaliano thabiti na ya kudumu
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kufikia makubaliano thabiti, ya kudumu na ya kutegemewa baina yake na kundi la 4+1 katika mazungumzo ya kujaribu kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA huko Vienna, Austria.
Ali Shamkhani amesema hayo hapa mjini Tehran katika mazungumzo yake na Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya (EU) na kuongeza kuwa, kama pande hizo zitakuwa na azma ya kweli ya kurejea kwenye JCPOA, basi Iran iko tayari kufikia mapatano.
Amesisitiza kuwa, Marekani kwa kutotekeleza majukumu yake, na Ulaya kwa kutowajibika kivitendo, zimevuruga fursa ya kunufaika na nia njema iliyodhihirishwa na Iran katika mazungumzo yaliyosita ya Vienna.
Shamkhani amesema hatua ya Iran kusimamisha utekelezaji wa hiari wa Itifaki ya Ziada ya Mkataba wa NPT, na hatua nyinginezo katika sekta yake ya nyuklia zinafanyika kwa mujibu wa sheria, na kwamba Tehran itaendelea kuchua hatua hizo iwapo Wamagharibi hawatabadilisha mienendo yao.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliingia katika mazungumzo ya Vienna kwa lengo la kuondolewa vikwazo, na kustafidi kiuchumi na mapatano ya JCPOA.
Kwa upande wake, Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya (EU) ameashiria vita vya Ukraine na kueleza kuwa, kuhuishwa mapatano ya JCPOA kutatakuwa na umuhimu mkubwa katika kuimarisha usalama wa eneo.
Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa EU amekosoa kitendo cha aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump cha kujitoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA.