Kamanda: Vikosi vya Jeshi la Iran vinaendelea kuimarika licha ya vikwazo
(last modified 2022-07-15T02:28:41+00:00 )
Jul 15, 2022 02:28 UTC
  • Kamanda: Vikosi vya Jeshi la Iran vinaendelea kuimarika licha ya vikwazo

Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Nchi Kavu la Iran amesema vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu vinendelea kuimarika na kupata nguvu zaidi siku baada ya siku, licha ya vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya taifa hili.

Brigedia Jenerali Yusuf Qorbani amesema hayo mjini Qazvin, kaskazini mwa nchi na kuongeza kuwa, "Tumekuwa chini ya vikwazo shadidi kwa zaidi ya miaka 40 sasa, lakini vikosi vyetu vya ulinzi vimeendelea kuwa na uwezo mkubwa."

Amesema maadui wameibua chokochoko na ghasia katika nchi zinazoiuzunguka Iran, lakini hawajaweza kuthubutu hata kufukiria tu kuitishia Jamhuri ya Kiislamu kutokana na nguvu kubwa za kijeshi za taifa hili.

Brigedia Jenerali Qorbani ameeleza bayana kuwa, hii leo vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vinatambulika kuwa na uwezo mkubwa kote duniani.

Askari wa US walivyoingiwa na kiwewe baada ya kambi ya Ain al-Asad kushambuliwa

Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Nchi Kavu la Iran ameashiria namna Iran ilivyovuurumisha makombora na kupiga kambi ya jeshi ya Marekani ya Ain al-Asad nchini Iraq baada ya kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani,  na kusisitiza kuwa Washington haikuwa na uthubutu wa kujibu shambulio hilo kwa kuwa linafahamu uwezo mkubwa wa kijeshi wa nchi hii.

Baada ya kipigo hicho cha Januari mwaka 2020, Marekani ilidai kuwa wanajeshi wake zaidi 100 waliokuwa katika kambi ya Ain al-Asad wamepata majeraha ya kisaikolojia, istilahi ambayo hutumiwa na Washington kupotosha au kuficha idadi ya askari wake waliouawa vitani.

 

 

Tags