Iran na Oman zajadili mapatano ya kuondolewa Tehran vikwazo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran inatathmini kwa kina jibu la serikali ya Marekani kuhusu masuala yaliyosalia katika mazungumzo ya kuliondolea vikwazo taifa hili.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Oman, Badr al-Busaidi ambapo wamejadili kuhusu matukio mapya yanayofungamana na nanma ya kufufuliwa mapatano ya kimataifa ya nyuklia maarufu kwa jina la JCPOA.
Amir-Abdollahian ameeleza bayana kuwa, Iran inachunguza majibu yaliyotolewa na Marekani kwa mapendekezo ya Umoja wa Ulaya kuhusu kufufuliwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA,
Amesisitiza kuwa, Iran itatangaza mtazamo wake na kutoa maamuzi baada ya kuyatathmini mapendekezo hayo ya Marekani.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema, "Tumejitolea kufikia makubaliano mazuri, ya kudumu na thabiti."
Duru mpya ya mazungumzo kuhusu kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, iliyoanza Agosti 4 mjini Vienna, ilimalizika Agosti 8. Katika duru hii ya mazungumzo, mapendekezo kadhaa yalitolewa na mratibu wa Umoja wa Ulaya katika mazungumzo ya Vienna.
Kwa upande wake, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Oman, Badr al-Busaidi amesema anatumai kuwa mazungumzo ya Vienna ya kuiondolea Iran vikwazo yatazaa matunda mazuri.