Salami: Maamuzi ya Iran yanaathiri uchaguzi wa Marekani
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema maamuzi ya kisiasa ya Jamhuri ya Kiislamu yana taathira na nafasi kubwa katika chaguzi za Marekani.
Brigedia Jenerali Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema hayo jana Jumanne akihutubia mkusanyiko wa Maprofesa wa jeshi la Basiji mjini Mashhad, kaskazini mashariki mwa nchi na kuongeza kuwa, hatima ya Ikulu ya White House huathiriwa moja kwa moja na Husseiniya ya Imam Khomeini, ambako Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu hufanya mikutano ya umma na kutoa hotuba zake.
Brigedia Jenerali Salami amesisitiza kuwa, mipango ghalati ya Marekani katika eneo hili la Asia Magharibi itafeli na kugonga mwamba. Ametahadharisha kuwa, stratejia hatari zaidi ambayo adui ameamua kutumia ni vita vya kinafasi na kisaikolojia.
Salami amesema: Asilimia 50 nguvu za kijeshi duniani inamilikiwa na Marekani, lakini bado (Wamarekani) wanakabiliwa na matatizo mengi ya ndani.

Kamanda Salami ameeleza bayana kuwa, hatua na uchokozi wowote wa adui utakabiliwa na jibu kali. Brigedia Jenerali Salami amesema, "Iran haitamuacha adui abakie hivi hivi na kwamba uchokozi wa adui utakabiliwa na jibu kali."
Kadhalika Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema wananchi wa Iran hawatafurahi na kushangilia kwa kuondolewa vikwazo haramu, na vilevile hawatashughulishwa na kubakishwa vikwazo hivyo, kwani Iran ni taifa huru.