Iran yasisitiza kukomeshwa chokochoko za utawala wa Kizayuni huko Syria
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa: Baraza la Usalama linapasa kuushinikiza utawala wa Kizayuni ili uhitimishe chokochoko na hatua zake za uvamizi dhidi ya mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Syria.
Amir Saeid Iravani amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu matukio ya kisiasa na kibinadamu huko Syria katika uga wa kisera na kusisitiza kuwa mgogoro wa Syria unapasa kupatiwa ufumbuzi kwa mujibu wa msingi wa kanuni na sheria za kimataifa. Amesema, ugaidi ungali ni tishio kuu huko Syria na katika eneo la Asia Magharibi; na kwamba uwepo wa vikosi vya nchi ajinabi kaskazini mwa Syria kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi ni kinyume na hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.
Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani vikali mashambulizi ya kigaidi yaliyotekelezwa tarehe 2 mwezi huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa huko Damascus mji mkuu wa Syria ambayo yanakinzana waziwazi na sheria za kimataifa kuhusu masuala ya kibinadamu na wakati huo huo yanauweka hatarini usalama na amani ya kikanda na kimataifa.
Iravani ameongeza kuwa, kwa kuzingatia hali mbaya ya kibinadamu huko Syria; Iran inaunga mkono kupasishwa kwa kauli moja azimio nambari 2672 mnamo tarehe 9 mwezi huu kwa lengo la kuongeza muda wa utaratibu wa kurefusha muhula kwa muda wa miezi mingine sita mingine kwa ajili ya masuala ya kibinadamu; na kwamba kitendo hicho ni hatua muhimu ili kuidhaminia Syria mahitaji ya haraka hasa kwa kuzingatia kuwa hali ya mazingira ya sasa ya msimu wa baridi kali.
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa aidha amesisitiza juu ya haja ya kuondolewa hatua za upande mmoja(vikwazo) dhidi ya wananchi wa Syria na akasema Syria ina nafasi na mchango muhimu katika eneo. Amesema Syria ni moja ya nguzo kuu ya amani na usalama katika Mashariki ya Kati.