"Uzoefu wa JCPOA umeipa Iran funzo la kutowategemea maajinabi"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93704-uzoefu_wa_jcpoa_umeipa_iran_funzo_la_kutowategemea_maajinabi
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema Jamhuri ya Kiislamu imejifunza kutowategemea maajinabi kutokana na uzoefu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2023 07:19 UTC

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amesema Jamhuri ya Kiislamu imejifunza kutowategemea maajinabi kutokana na uzoefu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Ali Baqeri Kani ambaye pia ni Mkuu wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia amesema hayo katika mahojiano na Press TV na kueleza kuwa, kutokana na upande wa pili kutoheshimu JCPOA na kusuasua mazungumzo ya kuhuisha mapatano hayo, taifa la Iran limepata somo la kuendelea kupiga hatua za ustawi na maendeleo, pasi na kuzitegemea nchi za nje.

Ameeleza bayana kuwa, upande wa pili wa mazungumzo hayo unaojumuisha Marekani na nchi za Ulaya ndio umefeli kutekeleza wajibu wao, na wameshindwa kuonyesha japo azma na irada njema ya kisiasa ya kuyahuisha mpatano hayo.

Amesisitiza kuwa, Iran imeendelea kushikamana na misimamo yake ya kuondolewa vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa kinyume cha sheria na itaendelea kusimama imara kupigania haki zake kwenye mazungumzo hayo.

Kani amebainisha kuwa, "Imethibiti kuwa, ikija katika suala la maslahi yao, Marekani na waitifaki wake wa Ulaya wanashindwa kuheshimu ahadi walizotoa, huku wakikanyaga misingi ya maadili."

Mazungumzo ya Vienna ya kuiondolea Iran vikwazo

Naibu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa vile vile amesisisiza kuwa, Tehran itaendelea kupigania kuondolewa vikwazo vyote vya kiuchumi ilivyowekewa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kinyume cha sheria.

Ali Baqeri Kani ameongeza kuwa, Iran imesalia katika mazungumzo hayo kwa lengo la kuhakikisha vikwazo haramu vya Marekani dhidi ya taifa hili vinaondolewa, mkabala wa Washington kuruhusiwa kurejea kwenye mapatano hayo.