Kiongozi Muadhamu azikosoa nchi za Waislamu kwa kufumbia macho kadhia ya Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94198-kiongozi_muadhamu_azikosoa_nchi_za_waislamu_kwa_kufumbia_macho_kadhia_ya_palestina
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezikosoa nchi za Kiislamu kwa kutochokua hatua yoyote ya maana juu ya kadhia ya Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 18, 2023 10:58 UTC
  • Kiongozi Muadhamu azikosoa nchi za Waislamu kwa kufumbia macho kadhia ya Palestina

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezikosoa nchi za Kiislamu kwa kutochokua hatua yoyote ya maana juu ya kadhia ya Palestina.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, "Palestina ingali kadhia kuu kwa umma wa Kiislamu. Taifa hilo limewekewa mzingiro kikamilifu na watu wasio wa kawaida, bali na kundi la watu waovu na mafasiki; hata hivyo nchi za Kiislamu zimeendelea kuwa watazamaji tu."

Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo leo Jumamosi hapa Tehran katika mkutano wake na maafisa pamoja na wajumbe wa nchi za Kiislamu walioshiriki kwenye Mashindano ya Kimataifa ya Qurani Tukufu. Mashindano hayo yamefanyika kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kubaathiwa na kupewa Utume, Mtume Muhammad (SAW).

Ayatullah Ali Khamenei amebainisha kuwa, kuendelea kufumbia macho na kunyamazia matatizo ya Wapalestina, na hata kushirikiana na utawala huo wa Kizayuni unaozikaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina kumezidhoofisha nchi za Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu ameyakosoa baadhi ya madola ya Kiarabu kwa kushindwa kusimama kidete mkabala wa utawala haramu wa Israel na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwaunga mkono kwa kila namna wananchi madhulumu wa Palestina.

Amefafanua kwa kusema: Kusalia kimya juu ya kadhia ya Palestina kumeudhuru ulimwengu wa Kiislamu. Kimya hicho cha serikali za Kiislamu mkabala wa uvamizi huo, ambao ni uvamizi pia dhidi yao na umma wa Kiislamu, na hata kuunga mkono (uvamizi huo), na baadhi wamefanya hivyo hivi karibuni, kumezidhoofisha nchi hizo na hata kuziweka katika madhila.

Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa, iwapo serikali za Kiislamu zingelisimama kidete juu ya kadhia ya Palestina tokea mwanzo na wapambane, basi hali katika eneo la Asia Magharibi bila shaka ingelikuwa tofauti, na umma wa Kiislamu leo hii ungelikuwa madhubuti na wenye umoja zaidi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuliunga mkono taifa la Palestina kwa njia zozote zile.

Akizungumzia utukufu wa Sikukuu ya Kubaathiwa Mtume (SAW), Ayatullah Khamenei amesema, Kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Mtukufu ilikuwa ni zawadi yenye thamani kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa jamii ya wanadamu.

Sanjari na kutoa mkono wa kheri na fanaka kwa Waislamu wote kote duniani kwa mnasaba huu adhimu, Kiongozi Muadhamu amesema ujumbe wa Mab'ath ya Mtume wa Allah (SAW) unamdhaminia mwanadamu Saada na mafanikio hapa duniani hadi Siku ya Kufufuliwa.