Iran, China na Russia zafanya luteka ya pamoja katika Bahari ya Oman
(last modified Thu, 16 Mar 2023 11:25:52 GMT )
Mar 16, 2023 11:25 UTC
  • Iran, China na Russia zafanya luteka ya pamoja katika Bahari ya Oman

Vikosi vya majini vya Iran, Russia na China vinaendelea na mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika Bahari ya Oman, huo ukiwa ni muendelezo wa juhudi za nchi tatu hizo za kuimarisha ushirikiano wa majeshi yao ya baharini.

Wizara ya Ulinzi wa Taifa ya China imesema maneva hayo ya kijeshi yatakayomalizika Machi 19, yanafanyika chini ya kaulimbiu ya 'Mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya 202 ya kuimarisha usalama wa njia za baharini'. 

Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, lengo la mazoezi hayo ya kijeshi ni kuimarisha kivitendo ushirikiano wa vikosi vya baharini vya nchi tatu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, China na Russia.

Katika luteka hiyo iliyoanza jana Machi 15, majeshi ya nchi hizo tatu yametumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushirikiana kuzima moto wa baharini, kuokoa chombo cha bahari kilichokuwa kimetekwa nyara, kushambulia maeneo maalumu pamoja na kufanya mashambulizi ya usiku dhidi ya vitu vya angani.

Vikosi vya majini vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, vikosi vya Jeshi la Majini la Iran, vikosi vya jeshi la Russia na vile vya Jeshi la Majini la China vinashiriki kwenye mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi.

Kuimarisha usalama wa biashara za bahari ya kimataifa, kupambana na maharamia na magaidi wa baharini, kubadilishana taarifa katika operesheni za uokoaji wa baharini, kubadilishana uzoefu wa kuendesha mbinu mbalimbali za kijeshi, ni miongoni mwa malengo ya luteka na mazoezi hayo ya kijeshi ya nchi tatu za Iran, China na Russia.

Oktoba mwaka jana, Admeli Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Baharini la Iran alisema kushiriki bega kwa bega Iran katika mazoezi kama hayo ya kijeshi na madola makubwa kama China na Russia ni ushahidi mwingine kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijatengwa licha ya vikwazo vikubwa vya kidhulma ilivyowekewa na Marekani. 

Tags