Apr 14, 2023 12:20 UTC
  • Mamilioni ya Wairani washiriki maandamano ya Siku ya Quds na kulaani jinai za Israel, Marekani

Mamilioni ya wananchi wa Iran ya Kiislamu leo ​​wameshiriki katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds na kuunga mkono mapambano ya ukombozi ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina ikiwa ni pamoja na kuonyesha kuchukizwa kwao na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wake hususan Marekani.

Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mjini Tehran yamehudhuriwa pia na maafisa wa serikali na jeshi chini ya kaulimbiu: “Palestina ni Mhimili wa Umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu; Quds Inakaribia Kukombolewa". Maandamano makubwa ya Siku ya Quds pia yamefanyika katika miji na vijiji zaidi ya elfu moja nchini Iran, sambamba na maeneo mengine ya dunia.

Mamilioni ya wananchi waliokuwa katika ibada ya Swaumu wa Tehran walikuwa wakipiga nara za "Mauti kwa Israeli na Mauti kwa Marekani", na kuonyesha kuchukizwa kwao na wahalifu hao. Vilevile wamewatangazia walimwengu jinsi watu wa Palestina wanavyoendelea kudhulumiwa na kuuawa kwa umati.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu yameakisiwa na zaidi ya waandishi wa habari na wapiga picha 4,000, wanaowakilisha mashirika 150 ya habari ya ndani na nje ya nchi.  

Baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa Iran walioshiriki katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds ni Rais Ebrahim Raisi, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu Mohammad Baqer Qalibaf, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama Hujjatul Islam Mohseni Ejei, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Ismail Qaani, na Waziri wa Ulinzi Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani.

Akizungumza katika maandamano hayo, Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa utawala wa Kizayuni unakaribia kusambaratika na kuongeza kuwa: Kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na baadhi ya nchi za Kiarabu hakutadhamini usalama wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Sayyid Ebrahim Raisi amesema maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds ni nembo ya mshikamano na umoja wa Umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa: "Quds tukufu inakaribia kukombolewa."

Rais Ebrahim Raisi katika maandamano ya Siku ya Quds

Akizungumzia ushiriki mkuwa wa wananchi wa Tehran katika maandamano ya Siku ya Quds, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema: Maandamano na mikusanyiko mikubwa inayofanyika katika Ulimwengu wa Kiislamu kuadhimisha siku hii ni nguzo muhimu ya uungaji mkono kwa watu wa Palestina, Lebanon na wapiganaji wa Jihadi wa kambi ya muqawama ili wajue kwamba hawako peke yao na kwamba watu wote wanawaunga mkono katika uwanja huu.

Imam Khomeini MA mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds. 

Waislamu na wapenda haki kote duniani wamekuwa wakifanya maandamano kila mwaka katika Siku ya Kimataifa ya Quds, na kuonyesha hasira zao dhidi ya siasa za kibaguzi za Israel na mshikamano wao na wananchi madhulumu wa Palestina.

Tags