Wanaoikalia Quds kwa mabavu wanakaribia kuanguka
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa ujumbe wa maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds ni kutangaza mshikamano na Umma wa Kiislamu na kwamba jitihada zinazofanywa na tawala za Kiarabu za kuhuisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel hazitadhamini usalama wa utawala huo.
Rais Ebrahim Raisi alisema siku ya Ijumaa pambizoni mwa maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa hapa Tehran kuwa maandamano hayo ni nembo ya mshikamano na umoja wa Umma wa Kiislamu na kwamba Quds Tukufu inakaribia kukombolewa.
Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu yamefanyika ili kutangaza mshikamano na wananchi wa Palestina huku maghasibu wa Kizayuni wakikabiliwa na mgogoro mkubwa zaidi ndani ya utawala huo haramu. Hii ni kwa sababu kuongezeka migogoro ndani ya utawala haramu wa Israel, kuimarika nguvu na nafasi ya wanamapambano na pia kupanuka mapambano ya raia wa Palestina hadi katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi kumeifanya hali ya mambo kuwa ngumu kwa Wazayuni maghasibu; na kama wanavyosema baadhi ya weledi wa mambo hali hiyo imeuweka utawala huo katika ncha ya kusambaratika.
Katika miezi ya karibuni duru za habari pia zimetoa ripoti mbalimbali kuhusu kusambaratika utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na sababu tofauti za ndani au za nje ya utawala huo. Kwa mfano, gazeti la Maariv limezinukuu duru za kijeshi na kuandika kuwa: Hali ya Israel ni mbaya na kwamba, kutolipuka kwa volcano hakuna maana kwamba lava za ndani yake hazitokoti.
Nukta muhimu kuhusu hali inayoukabili utawala wa Kizayuni ni kwamba, mbali na kupamba moto mapambano ya Wapalestina ambayo yamepanuka hadi katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan; hitilafu na migawanyiko ndani ya Wazayuni wenyewe na kati ya viongozi wa kisiasa wa utawala huo pia zinaongezeka kila uchao, na siasa za serikali ya Benjamin Netanyahu hasa kuhusu marekebisho sheria za mahakama, zimedhihirisha zaidi ufa na mgawanyiko ndani ya utawala huo haramu.
Miongoni mwa matokeo ya mgogoro wa sasa katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ni suala la kuhajiri Wazayuni katika ardhi zilizoghusubiwa za Palestina na kurudi katika nchi walikotokea. Kwa hakika, mgogoro wa sasa umesababisha sehemu kubwa ya Wazayuni wanaoishi katika ardhi hizo kufikiria kuhama na kurejea katika nchi zao za asili. Kuhusiana na suala hilo, taasisi ya Marekani ya IATI imefanya uchunguzi wa maoni kwa kushirikiana na shirika moja la Kizayuni ambapo matokeo ya uchunguzi huo mpya yameonyesha kuwa, asilimia 90 ya wajasiriamali na watendaji katika sekta ya teknolojia mpya ya utawala wa Kizayuni wanajaribu kuhamishia shughuli zao nje ya Israel kutokana na mazingira ya sasa yanaoukabili utawala wa Kizayuni.
Hapana shaka kuwa katika mazingira kama haya, utawala wa Kizayuni wa Israel kama ilivyokuwa huko nyuma, unafanya kila uwezalo kuzipotosha fikra za waliowengi ili kwa kiasi fulani kuficha ukubwa wa matatizo yake ya ndani. Aidha utawala wa Israel unatumia mashambulizi ya karibuni katika maeneo mbalimbali ya Palestina na maeneo Matukufu ya Waislamu na pia mashambulizi yake ya anga huko Syria kama moja ya hatua za kuficha migogoro yake ya ndani.
Pamoja na hayo, migogoro ya hivi sasa ya utawala wa Kizayuni ni zaidi ya hatua hizo za kufifiza au kurejesha utulivu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Kwa sababu pamoja na kukithiri kwa migogoro ya ndani, matukio ya kieneo pia yanakwenda kinyume na matakwa ya utawala huo. Kupunguzwa ushawishi wa Marekani katika eneo hili ambayo ni mshirika mkuu wa utawala wa Kizayuni, kuongezeka mafungamano baina ya nchi za Kiislamu na kutotaka kuanzisha uhusiano na utawala huu ni miongoni mwa matukio ambayo yameifanya hali kuwa ngumu zaidi kwa Wazayuni maghasibu.
Kwa hivyo, mwaka huu, Siku ya Kimataifa ya Quds imefanyika nchini Iran na katika nchi nyingine za dunia, ambapo majeshi ya muqawama ya Palestina na nchi za Kiislamu yamepata nguvu na kushikamana zaidi kuliko huko nyuma.
Kwa kuzingatia hali hiyo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema utawala wa Kizayuni unakaribia kusambaratika na kusisitiza kuwa: Idadi kubwa ya watu walioandamana katika Ulimwengu wa Kiislamu inadhihirisha kuangamia utawala wa Kizayuni na kukombolewa Quds Tukufu kulivyokaribia zaidi kuliko inavyodhaniwa."