Iran yampongeza Guterrez kwa kuunga mkono mazungumzo ya kikanda
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i97534-iran_yampongeza_guterrez_kwa_kuunga_mkono_mazungumzo_ya_kikanda
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wamefanya mazungumzo kuhusu matukio ya kikanda na kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 19, 2023 01:55 UTC
  • Iran yampongeza Guterrez kwa kuunga mkono mazungumzo ya kikanda

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wamefanya mazungumzo kuhusu matukio ya kikanda na kimataifa.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari la IRNA ambalo limesema, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, na huku akipongeza kikao cha hivi karibuni kilichoitishwa na Umoja wa Mataifa mjini Doha Qatar kwa ajili ya kuzungumzia kadhia ya Afghanistan, kwa ubunifu wa Guterres, amesema, wakimbizi wa Kiafghani walioko nchini Iran wanafika milioni tano na kwamba kuwasimamia na kuwahudumia wakimbizi wengi kiasi chote hicho lazima kunahitaji msaada na uungaji mkono wa kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amempongeza pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kuunga mkono mazungumzo ya kikanda na kuelezea matumaini yake ya kuona vita vya Yemen vinamalizika kikamilifu, vikwazo vyote vinaondolewa na vita vya Ukraine navyo vinakomweshwa mara moja. 

Amesema, tunatamani kuziona Russia na Ukraine zinarejea kwenye mkondo wa mazungumzo ya maana ambayo yatapelekea kumalizika vita huko Ukraine. 

Wakimbizi wa Afghanistan nchini Iran wanapewa haki zao zote zikiwemo za elimu bora

 

Amma kuhusu jinai za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni huko Ghaza, Amir-Abdollahian amesema, vita hivyo vya siku tano na jinai kubwa isiyo na chembe ya ubinadamu iliyofanywa na Wazayuni kwenye vita hivyo dhidi ya Wapalestina kamwe haviwezi kunyamaziwa kimya na makundi ya muqawama ya Palestina na daima yataendelea kupata majibu makali.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameishukuru Iran kwa kupokea mamilioni ya wakimbizi kutoka Afghanistan na amesisitizia haja ya kusaidiwa Jamhuri ya Kiislamu katika kuwahudumia wakimbizi hao. Ameelezea matumaini yake pia ya kumalizika vita vya Ukraine, kupatikana usitishaji vita wa kudumu wa vita vya Yemen, kupatikana amani Afghanistan na kuongezeka ushirikiano wa kimataifa katika vita dhidi ya ugaidi.