Idadi ya watalii wanaoitembelea Iran yaongezeka kwa asilimia 300
Shirika la Kimataifa la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO) limesema zaidi ya watalii milioni 4.1 waliitembelea Iran mwaka jana 2022, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 315 ikilinganishwa na mwaka juzi 2021.
Gazeti la Financial Tribune limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, ongezeko hilo la idadi ya watalii wanaoitembelea Jamhuri ya Kiislamu yumkini limetokana na kuondolewa hatua na sheria kali zilizokuwa zimewekwa na nchi nyingi duniani kwa lengo la kudhibiti msambao wa ugonjwa wa COVID-19.
Mwaka 2019 kabla ya janga la Corona, Iran ilishuhudia idadi kubwa zaidi ya watalii kuwahi kuitembelea nchi hii katika miaka ya karibuni, ambapo iliwapokea watalii zaidi ya milioni 9.
Mwaka 2020 kutokana na vizingiti vya Corona, sekta ya utalii ilipungua kwa asilimia 50 lakini mwaka 2021 baada ya kupunguzwa vizingiti vya Corona, sekta hiyo ilianza kustawi tena na pato lake kupindukia mabilioni ya dola.
Mchango wa utalii katika uchumi wa Iran mwaka 2020 ulikuwa ni asilimia 3 na kiwango hicho kiliongezeka na kupindukia asilimia nne mwaka 2021. Kufuatia kuongezeka idadi ya watalii, sekta ya ajira nayo pia imeweza kustawi nchini Iran.
Iran ni nchi yenye ustaarabu mkongwe na hivyo ina vivutio vingi vya kitalii kwa wapendao historia. Aidha Iran ina vivutio vingi ya Kiislamu hasa maeneo ya ziara ambayo hutumbelewa na Waislamu kama vile Haram Takatifu ya Imam Ridha AS mjini Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran na Haram Takatifu ya Bibi Maasuma SA katika mji wa Qum kusini mwa Tehran.