Imam Khomeini; shakhsia wa kimataifa na nembo ya kupinga ubeberu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i98402-imam_khomeini_shakhsia_wa_kimataifa_na_nembo_ya_kupinga_ubeberu
Jumapili ya jana ilisadifiana na siku ya kukumbuka kifo cha Imam Khomeini (MA), mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jun 04, 2023 23:03 UTC
  • Imam Khomeini; shakhsia wa kimataifa na nembo ya kupinga ubeberu

Jumapili ya jana ilisadifiana na siku ya kukumbuka kifo cha Imam Khomeini (MA), mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi huyo aliutikisa ulimwengu kwa fikra zake huru na uongozi wake wa kishujaa katika kilele cha Vita Baridi mwishoni mwa miaka ya 70 na hivyo kuibua damu mpya katika harakati za Kiislamu na za kupigania uhuru duniani. Kwa msingi huo, Imam Khomeini si tu ni shakhsia anayeheshimika kimatiafa na kupendwa na walimwengu, bali mitazamo na fikra zake za kupambana na dhulma na ubeberu ni jambo linaloenziwa sana na kufuatwa na wapigania haki na uhuru ulimwenguni.

Kuhusiana na suala hilo, Tajammul Hosseini, Mkuu wa Harakati ya Shahidi Hosseini ya nchini Pakistani huku akifafanua kwamba Imam Khomeini (MA) alifanikiwa pakubwa na kuweza kuweka mfano mzuri wa kufuatwa katika jamii ya Kiislamu kutokana na busara na ikhlasi yake, amesisitiza kuwa athari za mfano huo ni suala linaloonekana wazi miongoni mwa harakati za kupigania uhuru na ukombozi duniani. Anasema kwa msingi huo tunaweza kusema bila kusita kwamba mfungamano mkubwa uliopo kati ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na thamani za Kiislamu na vilevile fikra za mafundisho ya Kiislamu za Imam Khomneini (MA) ndicho chanzo kikuu cha kuendelea kudumu fikra za Kiongozi huyo mashuhuri wa Kiislamu. Kwa msingi huo, njia na fikra za Imam (MA) katika kukabiliana na uistikbari na ubeberu wa madola ya Magharibi, fikra ambazo bila shaka zinatokana na mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu, zimeweza kuvuka mipaka na kuwavutia walimwengu wa mataifa tofauti, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya madola hayo na hivyo kuyatia wasiwasi mkubwa.

Waombolezaji wakiwa katika Haram ya Imam Khomeini (MA)

Maulana Qamar Hasnain, Mkurugenzi wa Jamaat al-Fatima (as) ya India, anasema katika mwelekeo huo huo mkwamba: "Historia na maisha ya Imam Khomeini (MA) yana mafunzo mengi na ujumbe aliouwasilisha kwa ulimwengu ni muhimu sana na wenye taathira kubwa ambazo zingalipo hadi leo. Miongoni mwa ujumbe wake muhimu zaidi ni tangazo la Siku ya Quds la kuiunga mkono Palestina kwa hoja kuwa Quds na ardhi za Palestina zinapaswa kuwa huru na kuwa Waislamu wote wanawajibika kuungana kwa ajili ya kufikia lengo hilo."

Hilo ndilo jambo linalowafanya Wazayuni wanaoikalia kwa mabavu ardhi za Palestina waingiwe na wasiwasi mkubwa na kufanya kila wanaloweza kwa ajili ya kupinga kuenea ulimwenguni fikra za Imam. Hiyo ndio maana wamekuwa wakitekeleza kwa makusudi siasa za jinai na ukandamizaji dhidi ya makundi ya Wapalestina wasio na hatia ili fikra za Imam zisiweze kuandaa mazingira ya maghasibu hao wa Kizayuni kupata mapigo makubwa zaidi kutoka kwa Wapalestina na Waislamu kwa ujumla.

Imtiaz Razavi, mhadhiri wa chuo kikuu na mwanaharakati wa kijamii wa Pakistani anatathmini upeo wa kimataifa wa mbinu na fikra za Imam katika kupambana na ubeberu na udhalimu wa madola ya kikoloni ya Magharibi na kusema: "Kupitia ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini (MA) aliweza kuamsha umma wa Kiislamu na kuandaa mazingira ya kusaidiwa wanyonge duniani na wakati huo huo kuwahamasisha Waislamu dhidi ya ubeberu wa kimataifa. Kupitia ujumbe huo aliweza kuwathibitishia kwamba ubeberu na dhulma kamwe havidumu, na kwamba hatupasi kujidhalilisha na kukubali matakwa haramu ya maadui, bali tunapasa kupambana nao kwa ajili ya kueneza uadilifu duniani." Maulana Mazhar Abbas Ghazi, mmoja wa maulama wanaharakati wa mjini New Delhi nchini India, anaamini kwamba Imam Khomeini (R.A.) alianzisha mapinduzi makubwa, ambayo hayajawahi kuonekana tena duniani.

Ayatullah Khamenei akiwahutubia waombolezi katika Haram ya Imam Khomeini (MA)

Anasema: "Sisi mjini New Delhi na Waislamu wote duniani tumeathirika na shakhsia ya Imam Khomeini. Hili ni jambo la kushangaza sana. Muasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa shakhsia na mchamungu mkubwa ambaye alikuwa hajawahi kuonekana katika zama za karibuni. Alikuzwa na kulelewa katika mazingira ya kiroho kiasi kwamba alikuwa na nafasi kubwa katika masuala ya kielimu, ujasiri, thamani za kimaadili na nyanja nyingine nyingi. Kwa vyovyote vile, Imam Khomeini (MA) si shakhisia wa zama wala kizazi kimoja tu. Kwa fikra zake zilizosimama juu ya msingi wa mafundisho ya Uislamu, alithibitisha kuwa kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu watu wanaweza kukabiliana kwa ushujaa na hatimaye kuwashinda madhalimu bila matatizo makubwa. Hilo ni jambo ambalo limekaririwa na kuthibitishwa kivitendo katika historia ya mwanadamu. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa madamu historia itaendelea kuwa hai, fikra na mawazo ya Imam Khomeini (MA) pia yataendela kuwa hai."