Alamolhoda: Marekani inaihujumu Iran kwa kutumia udikteta wa vyombo vya habari
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i98846-alamolhoda_marekani_inaihujumu_iran_kwa_kutumia_udikteta_wa_vyombo_vya_habari
Mke wa Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema Marekani, ambayo ilikuwa ikiunga mkono tawala za kiimla hapa nchini huko nyuma, hivi sasa inaifanyia hujuma Jamhuri ya Kiislamu kwa kutumia udikteta wa vyombo vya habari.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jun 16, 2023 04:15 UTC
  • Alamolhoda: Marekani inaihujumu Iran kwa kutumia udikteta wa vyombo vya habari

Mke wa Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema Marekani, ambayo ilikuwa ikiunga mkono tawala za kiimla hapa nchini huko nyuma, hivi sasa inaifanyia hujuma Jamhuri ya Kiislamu kwa kutumia udikteta wa vyombo vya habari.

Jamileh Alamolhoda alisema hayo katika mahojiano na televisheni ya Venezuela ya Telesur na kuongeza kuwa, "Ni vyema kuashiria kuwa, Marekani kwa miaka mingi iliunga mkono udikteta hapa nchini."

Alamolhoda ameeleza kuwa, historia inajikariri hivi sasa, kwani wale ambao waliunga mkono na kuuhami udikteta katika utawala wa Pahlavi kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979 nchini Iran, hii leo wanatumia vyombo vya habari kuwafanyia udikteta Wairani.

Mama wa Taifa wa Iran ameashiria namna vyombo vya habari vya Marekani vilivyoteka nyara na kupotosha habari za kifo cha msichana wa Kiirani, Mahsa Amini na kueleza kuwa, binti huyo aliaga dunia kutokana na mshtuko wa moyo Septemba mwaka jana, kwa mujibu wa uchunguzi na ripoti za madaktari.

Rais wa Iran akiondoka Cuba

Alamolhoda ambaye alikuwa ameandamana na Rais Raisi katika ziara yake ya kuzitembelea nchi tatu za Amerika ya Latini za Venezuela, Nicaragua na Cuba amesema, "Vyombo vya habari (vya Wamagharibi) vilivalia njuga kifo hicho na kukitumia dhidi ya wananchi, nchi, mfumo, viongozi na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran."

Jamileh Alamolhoda, Mke wa Rais Ebrahim Raisi ameongeza kuwa, Iran kama nchi yenye ustaarabu mkongwe wa miaka 15,000, imefanikiwa kusimama kidete dhidi ya jitihada za kibeberu za Marekani, na ndiposa "Wairani wanachekelea jitihada hizo zilizofeli za Wamarekani."