Kan'ani: Mtazamo, misimamo ya Iran kwa Marekani haibadiliki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99226-kan'ani_mtazamo_misimamo_ya_iran_kwa_marekani_haibadiliki
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mtazamo na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu kwa Marekani ipo wazi kabisa na haibadiliki, na inaweza kubadilika tu iwapo Washington itakomesha kikamilifu mienendo yake ya kiuhasama dhidi ya taifa hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 26, 2023 07:47 UTC
  • Kan'ani: Mtazamo, misimamo ya Iran kwa Marekani haibadiliki

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mtazamo na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu kwa Marekani ipo wazi kabisa na haibadiliki, na inaweza kubadilika tu iwapo Washington itakomesha kikamilifu mienendo yake ya kiuhasama dhidi ya taifa hili.

Nasser Kan'ani amesema hayo leo katika kikao cha wiki na waandishi wa habari hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, kamwe Iran haitafungamanisha maslahi na sera zake za nje na misimamo ya nchi fulani.

Amesema, "Mtazamo wa Iran kwa Marekani unatokana na msingi wa hulka yao ya kiuadui, na ni wazi kuwa misimamo ya Tehran kwa Washington haitobadilika mpaka pale Wamarekani watakapobadilisha kikamilifu mienendo yao ya kiuadui dhidi ya Wairani." 

Kan'ani amesema Iran inaingia katika Wiki ya Haki za Binadamu za Kimarekani, na kwamba ameandaa orodha ya sehemu ndogo ya maelfu ya jinai za Marekani kwa wananchi wa Iran. Amesema Marekani inastahili kubebeshwa dhima ya jinai za kutisha ilizofanyia Wairani.

Kan'ani ameeleza bayana kuwa, msimamo wa serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa na uhusiano wenye mlingano na nchi mbalimbali, kwa misingi ya pande husika kuheshimiana.

Kwengineko katika kikao hicho na waandishi wa habari hapa mjini Tehran, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mustakabali wa uhusiano wa kiuchumi baina ya Iran na Saudi Arabia unang'aa na unatia matumaini. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Iran na Saudi Arabia zina fremu ya kuridhisha ya kupanua ushirikiano wao wa kiuchumi na kibiashara, ili ushirikiano huo uendane na kuimarika uhusiano wa kisiasa wa Riyadh na Tehran.

Kuhusu ripoti za baadhi ya vyombo vya habari za eti kufikiwa mapatano ya siri kati ya Iran na Marekani, Nasser Kan'ani amesema, "Hatuwezi kusema chochote kuhusiana na uvumi wa baadhi ya vyombo vya habari. Iran inaendelea kufungamana na mchakato wa mazungumzo ili kupigania haki za taifa la Iran."