Oct 04, 2023 12:36 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni wauvamia Msikiti wa Al Aqswa kwa siku ya tano mfululizo

Makumi ya walowezi wa Kizayuni leo wameuvamia tena kwa siku ya tano mtawalia Msikiti wa Al-Aqwsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu huku wakilindwa na kusindikizwa na askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Ripoti zinasema kuwa, idadi kubwa ya walowezi wa Kizayuni wamevamia eneo hilo takatifu na kufanya vitendo vya kichochezi.

Msikiti wa al-Aqswa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa eneo takatifu la Quds na utawala wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo, lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kupelekea njama zake kushindwa.

Walowezi wengi wa Kizayuni wenye misimamo mikali mara kwa mara wamekuwa wakivamia msikiti wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu na kufanya vitendo vya kichochezi huku wakiwa wanapatiwa ulinzi na vikosi vya usalama vya utawala haramu wa Israel.

Walowezi wa Kizayuni

 

Vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Tangu serikali ya Waziri Mkuu Benjamini Netanyahu ishike tena hatamu za uongozi, huko Israel, hujuma na uvamizi wa mara kwa mara wa walowezi wa Kizayuni umechukua mkondo mpana zaidi.

Tags