Dec 18, 2023 10:19 UTC
  • Mashambulio ya anga ya Israel yaua Wapalestina 100 Jabalia

Wapalestina zaidi ya 100 wameuawa shahidi katika mashambulizi mapya ya utawala wa Kizayuni wa Israel yaliyolenga kambi ya wakimbizi ya Jabalia katika Ukanda wa Gaza.

Kanali ya Press TV imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, watu zaidi ya 100 wangali wamefukiwa kwenye vifusi vya majengo yaliyolengwa na mabomu ya Israel katika hujuma hiyo. 

Wizara ya Afya huko Gaza imesema makumi ya watu wamejeruhiwa na kwamba yumkini idadi ya wahanga wa mashambulizi hayo ya kinyama ikaonegezeka kutokana na hali mbaya ya majeruhi.

Kanali ya al-Mayadeen imeripoti kuwa, miongoni mwa waliouawa shahidi katika hujuma hiyo mpya ni Dina Abu Muhsen, ambaye wazazi na ndugu zake wawili waliuawa huko nyuma katika mashambulizi mengine ya Wazayuni. 

Habari zaidi zinasema kuwa, kambi ya wakimbizi ya Jabalia ambayo ndiyo kubwa zaidi Gaza imeharibiwa vibaya kutokana na shambulio hilo la bomu la Wazayuni.

Utawala wa Kizayuni umeshambulia mara kadhaa kambi hiyo ya wakimbizi, tangu uanzishe hujuma zake za kinyama dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Jana Jumapili, jeshi katili la Israel lilishambulia Hospitali ya al-Awda katika eneo la Jabalia na kuwateka nyara wafanyakazi kadhaa.

Mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, Wapalestina zaidi ya 200 waliuawa shahidi katika shambulizi jingine la utawala wa Kizayuni wa Israel lililolenga kambi hiyo ya wakimbizi.

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kwamba, idadi ya mashahidi wa Kipalestina tangu kuanza hujuma za utawala wa Kizayuni huko Gaza mnamo Oktoba 7 imepindukia watu 20,000.

Tags