Jan 04, 2024 02:43 UTC
  • Benki Kuu ya Israel: Vita vya Ghaza vinazidi kututia hasara, itafika dola bilioni 58

Gavana wa Benki Kuu ya Israel amesema kuwa vita vya Ghaza vinazidi kutia hasara utawala wa Kizayuni na hasara hizo zinaweza kupindukia dola bilioni 58 za Kimarekani.

Hayo yameripotiwa na tovuti ya habari ya Ma'an ambayo imemnukuu Amir Yaron, Gavana wa Benki Kuu ya utawala wa Kizayuni akisema kuwa, tunatabiri kwamba hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024 na 2025, kiwango cha deni la Israel kitaongezeka kwa asilimia 66 katika pato lake ghafi. 

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa utabiri wa Benki Kuu ya Israel, gharama na hasara za vita vya Ghaza kwa utawala wa Kizayuni itapindukia dola bilioni 58 za Kimarekani.

Gavana huyo wa Benki Kuu ya utawala wa Kizayuni ameonya pia kuwa, kama hakutachukuliwa hatua za haraka za kuokoa bajeti  ya Israel ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya vita vya Ghaza na kuvunjwa baadhi ya wizara, hasara itakazopata Israel zitakuwa kubwa mno.

Majeneza ya wanajeshi makatili wa Israel walioangamizwa kwenye vita na wanamapambano wa Palestina

 

Wakati huo huo serikali ya Joe Biden huko Marekani haijachukua hatua yoyote isipokuwa kutishia tu kupunguza misaada ya kijeshi kwa utawala wa Kizayuni. 

Wizara ya Vita vya Israel ilikuwa imetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni umeshatumia zaidi ya aina elfu 10 za silaha za kijeshi za Marekani dhidi ya wananchi wa Ghaza tangu tarehe 7 Oktoba 2023.

Marekani imetangaza wazi kuwa, misaada na uungaji mkono wake kwa jinai za Israel hautetereki huku utawala wa Kizayuni nao haujali mashinikizo yoyote ya kimtaifa bali unaendelea kutenda jinai za kutisha dhidi ya wananchi wasio na hatia huko Ghaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kutokana na uungaji mkono kama huo wa madola ya kibeberu hasa Marekani.

Tags